Hisia mseto serikalini Kiunjuri kupigwa kalamu
Na CHARLES WASONGA
WANDANI wa Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto wametoa hisia kinzani kuhusu mabadaliko ambayo Rais alifanyia baraza lake la mawaziri, haswa kufutwa kwa Mwangi Kiunjuri kama Waziri wa Kilimo.
Nao wandani wa kiongozi wa ODM, Raila Odinga wamepongeza hatua hiyo wakisema itaimarisha utendakazi serikalini.
Mbunge Maalum Maina Kamanda, ambaye ni wa mrengo wa ‘Kieleweke’, alisema kufutwa kwa Bw Kiunjuri kulijiri wakati ufaao, akisema waziri huyo amekuwa akitumia muda wake mwingi kumfanyia kampeni Dkt Ruto badala ya kushughulikia masuala ya wizara yake.
Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru na Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu pia waliunga mkono mabadiliko hayo wakielezea matumaini kuwa walioteulwia wataweka kando siasa na kuwahudumia Wakenya.
Lakini Seneta wa Nandi, Samson Cherargei na Mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro walidai Rais hakutenda “haki” kwa kumfuta kazi Bw Kiunjuri kwa kujiingiza katika siasa kama inavyodaiwa.
“Ikiwa Rais alipaswa kuwafuta kazi mawaziri wanaojihusisha na siasa basi angeanza na mawaziri Fred Matiang’i (Usalama), Eugene Wamalwa (Ugatuzi) na Peter Munya. Lakini kwa kumlenga Kiunjuri pekee ni uonevu mkubwa,” akasema Seneta Cherargei.
Na Bw Nyoro akaongeza: “Dkt Matiang’i anatumia muda wake mwingi kuchapa siasa ya BBI ilhali magaidi wa Al Shabaab wanawaua polisi na wananchi eneo la Kaskazini Mashariki na Pwani kila siku.”
Wakati huo huo, wabunge wa ‘Tangatanga’ kutoka eneo la magharibi mwa Kenya wamelalamikia kile wanachotaja kama kupuuzwa kwa eneo hilo katika teuzi mpya ambazo Rais Kenyatta alifanya jana.
Walidai waliofaidi ni watu kutoka eneo la Nyanza ambao hawakumpigia kura kwa wingi katika uchaguzi mkuu wa 2017 kama watu wa Magharibi.
“Japo watu wetu walipigia Jubilee kura kwa wingi kuliko wale wa Nyanza, tunasikitika kuwa Rais Kenyatta hajateua mtu kutoka jamii yetu ya magharibi katika orodha aliyosoma leo (jana) akiwa Mombasa.
Ni watu wa Raila ndio wameteuliwa hawakumpigia kura uchaguzi uliopita,” Mbunge Sirisia John Waluke akawaambia wanahabari katika majengo ya bunge, Nairobi, jana.
Aliandama na wenzake Didmus Barasa (Kimilili), Dan Wanyama (Webuye Magharibi) na kiranja wa wengi bunge Benjamin Washiali (Mumias Mashariki).
Katika mabadiliko ambayo Rais Kenyatta alitangaza jana katika mawaziri, mawaziri wasaidizi na makatibu wa wizara, aliyekuwa Mbunge wa Nyakach Peter Odoyo aliteuliwa kuwa Waziri Msaidizi wa Ulinzi huku Afisa Mkuu Mtendaji wa Taasisi wa Kuandaa Mitaala Nchini (KICD) Dkt Jwan Ouma akiteuliwa kuwa Katibu wa Wizara anayesimamia Mafunzo ya Kiufundi.
Bw Barasa alidai kuwa wawili hawa na watu wengine kutoka Nyanza, miongoni mwa wengine, waliteuliwa kwa sababu na ushawishi wa kiongozi wa ODM Raila Odinga kutokana na uhusiano wake wa karibu na Rais baada ya wawili hao kuridhiani kisiasa mnamo Machi 9, 2018.
“Hii handisheki kati ya Raila na Uhuru ndio sasa imepelekea watu wetu kukosa viti katika serikali hii ambayo tuliipigania kwa nguvu zetu zote. Rais hafai kutusau ilihali ni sisi tulimsaidia wakati Raila na watu wake walisusia marudio ya uchaguzi Oktoba 26, 2017,” akasema.
Hata hivyo, Bw Washiali alikataa kuzungumzia suala hilo akisema Rais ana mamlaka ya kufanya mabadiliko na teuzi katika serikali yake anavyotaka.
“Nadhani Rais Kenyatta aliongozwa na busara katika mabadilika na teuzi aliyofanya leo (jana). Naamini walioteuliwa wataendeleza ajenda ya maendeleo ya Jubilee.Siwezi kumkosoa Rais kwa sababu ni bosi wangu,” akasema.