Hofu baada ya wanaume kuonywa na vijana watatahiriwa
Na GERALD BWISA
WANAUME kutoka jamii zisizopasha tohara wanaoishi katika Kaunti ya Trans Nzoia wana hofu baada ya kuonywa na vijana wa eneo hilo kwamba watatahiriwa kwa lazima kwa msingi wa tamaduni za jamii ya Wabukusu.
Wanaume hao ambao wengi ni wa jamii za Waluo, Waturkana na Wateso walisema kuna vijana ambao wameanza kufanya msako kuwalazimisha wapashwe tohara.
Walisema huwa wanalazimika kutoroka makwao kila mwaka ifikapo msimu wa Wabukusu kupeleka wavulana jandoni kwani wanalazimishwa kufanya kitu kisicho na maana yoyote katika tamaduni zao.
“Unatarajiaje mwanamume mzee anayepaswa kuitwa babu atahiriwe kwa lazima? Nina watoto wanane na wake wawili na nimeishi hivi maisha yangu yote, utasemaje mimi si mwanamume?” akashangaa Bw George Odhiambo, 45, ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kipsongo.
Bw Odhiambo alilazimika kuhamia eneo salama baada ya kundi la vijana waliokuwa wakipita karibu na boma lake kutishia kumtahiri pamoja na wanawe watano kabla Agosti itamatike.
“Wake wangu na watoto watafikiriaje wakiona mwanaume ambaye wanamfahamu kuwa mkuu wa familia yao akitahiriwa katika umri huu? Hizo si utamaduni wala imani yetu. Hatua hiyo ni ukiukaji wa haki za binadamu,” akasema.
Bw Peter Etyang, 33, aliambia wanahabari kuwa anahama kutoka mtaa wa mabanda wa Kipsongo pamoja na wanawe wawili baada ya vijana kutishia kuwatahiri kwa lazima.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Trans Nzoia, Bw Samson ole Kine, alisema hakuna mtu yeyote ambaye amewasilisha malalamishi kama hayo kwa polisi lakini akaahidi watachunguza suala hilo na yeyote atakayepatikana akihangaisha wengine atakamatwa.
“Sioni umuhimu wowote wa kutahiriwa katika umri wangu ilhali mke wangu hajawahi kulalamika kuhusu nilivyo wakati wowote. Tumeamua kwenda kwetu Busia kwa sababu hawa vijana wa Kibukusu huwa hawafanyi utani,” akasema.
Alisema tangu alipohamia kaunti hiyo mapema miaka ya 1990, hajawahi kuishi kwa amani kila wakati msimu wa tohara unapofika na kuna wakati alishuhudia rafiki yake akitahiriwa kwa lazima.
Mkazi mwingine, Bw Evans Tido, 40, alilazimika kumhamisha mpwa, wa miaka 18 kurudi Turkana baada ya kuhangaishwa na vijana waliotaka kumtahiri kwa lazima kando ya barabara.
Katika mwaka wa 2016, wanaume zaidi ya 12 kutoka jamii ya Waturkana walitahiriwa kwa lazima na kulazimu mashirika ya kutetea haki za binadamu katika kaunti hiyo yaingilie kati.