Hofu huku maambukizi ya corona yakizidi
COLLINS OMULO na CHARLES WASONGA
WAZIRI wa Afya Mutahi Kagwe amewaonya wanasiasa dhidi ya kuandaa mikutano ya kisiasa huku 685 zaidi wakithibitishwa kuwa na virusi vya corona Jumapili.
Hii ni baada ya sampuli kutoka jumla ya watu 4,912 kupimwa ndani ya saa 24.
Akiongea na wanahabari katika makao makuu ya Wizara ya Afya, Nairobi baada ya kuongoza mkutano wa Kamati ya Kitaifa ya Kupambana na Janga hilo (NERC), Bw Kagwe alitangaza kuwa watu saba zaidi wamefariki kutokana na ugonjwa huo.
Alisema idadi ya maambukizi mapya iliyoandikishwa jana inaashiria kuwa kiwango cha maambukizi kimepanda hadi asilimia 12 kutoka asilimia 4 Septemba serikali ilipolegeza masharti ya kuzuia msambao wa virusi hivyo.
“Hii ina maana kuwa Wakenya haswa wanasiasa wameanza kupuuza masharti ya kudhibiti ugonjwa hali ambayo inaelekea kuchochea wimbi la pili la maambukizi. Nawaomba wananchi, haswa viongozi wa kisiasa kukomesha mikutano ya hadhara na wananchi wakome kuwazingira viongozi popote wanapoenda,” akasema Bw Kagwe.
Wakati huo huo, wakazi zaidi ya 2,000 wa Nairobi wamepimwa Covid-19 katika awamu ya pili ya shughuli ya kupima iwapo wameambukizwa, bila malipo, iliyozinduliwa na Idara ya Huduma za Jiji la Nairobi (NMS) mwishoni mwa wiki.
Mchakato huo wa upimaji wa halaiki uliendeshwa katika maeneobunge yote 17 ya Nairobi ambapo jumla ya watu 2,054 walipimwa katika siku ya kwanza mnamo Jumamosi huku kukiwa na dalili za kuzuka kwa wimbi la pili la maambukizi.
Eneo bunge la Makadara ndilo lilishuhudia idadi kubwa ya waliojitokeza kwa shughuli hiyo ambapo watu 247 walipimwa. Kibra ilifuatia kwa watu 214, Dagoretti Kaskazini (168), Kamukunji (140), Embakasi Kaskazini (135), Kasarani (125), Westlands (124) huku Embakasi Kusini ikiandikisha watu 120.
Watu wengine 106 walipimwa katika Embakasi Magharibi, Lang’ata (100), Embakasi ya Kati (96), Embakasi Mashariki (95), Ruaraka (82), Starehe (81), Mathare (80), Roysambu (72) na Dagoreti Kusini (69).
Sampuli za watu hao sasa zitapelekwa katika Hospitali ya Mama Lucy Kibaki, ili zipimwe katika maabara.