Habari MsetoSiasa

Hofu mgomo wa watumishi wa kaunti ukinukia

August 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

DERICK LUVEGA na BENSON AMADALA

VIONGOZI wameeleza hofu yao kuhusu mgomo wa wafanyakazi wa kaunti ambao umepangiwa kuanza Jumanne.

Kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi amewataka wabunge na maseneta kuandaa mazungumzo ili kusuluhisha utata kuhusu mswada wa ugavi wa mapato ili wafanyakazi wa kaunti walipwe mshahara wao wa mwezi Julai ndipo wafutilie mbali mgomo huo unaotarajiwa kukumba karibu kaunti zote 47.

“Naomba Bunge la Kitaifa na lile la Seneti kuandaa mazungumzo na kusuluhisha utata kuhusu mswada wa ugavi wa mapato. Jinsi tunavyoendelea na tofauti hizi ndivyo wafanyakazi wa kaunti wanavyoendelea kuumia,” akasema Bw Mudavadi.

Huku Bunge la Kitaifa likipigia upatu mswada unaopendekeza mgao wa Sh316 bilioni kwa kaunti, Bunge la Seneti limeshikilia kwamba kiasi hicho lazima kiwe Sh335 bilioni liwalo na liwe.

Ishara ya mgomo ilianza wiki jana baada ya Muungano wa Wafanyakazi wa Kaunti nchini kutangaza kuwa wanachama wao wataanza mgomo leo iwapo hawatakuwa wamelipwa mshahara wao wa Julai.

Mnamo Jumamosi, Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Wycliffe Oparanya aliwakashifu wabunge kwa kuhujumu utendakazi wa kaunti baada ya kukataa kupitisha mswada wa bunge la seneti unaopendekeza nyongeza kwenye mgao wa fedha zilizotengewa serikali za ugatuzi mwaka huu.

Huku Seneti na Bunge la Kitaifa zikiendelea kushikilia misimamo yao mikali, sekta ya afya ndiyo itakayoathirika zaidi iwapo Muungano wa Kitaifa wa Wauguzi (KNUN) utawatangazia wanachama wao waanze mgomo.

Rais Uhuru Kenyatta naye mwezi uliopita alisema serikali haina pesa za kuongezea kaunti huku magavana nao wakielekea Mahakama ya Juu kupata suluhu kwa zogo la ugavi wa mapato kati ya seneti na bunge la kitaifa.

Akizungumza kwenye hafla tofauti, Gavana wa Vihiga Dkt Wilber Ottichilo alieleza hofu yake kwamba wauguzi katika kaunti hiyo wataandaa mgomo baada ya kukamilika kwa notisi waliyotoa kwa utawala wake.

Alidai kuwa hii inatokana na kucheleweshwa kwa mshahara wao wa mwezi jana.

“Wauguzi wametishia kuandaa mgomo kuanzia kesho iwapo hawatakuwa wamelipwa mshahara wao. Iwapo hili litatokea basi watu wetu watafariki. Nawaomba wabunge wakubaliane na kupitisha mswada wa ugavi wa mapato,” akasema Dkt Otichillo ambaye alifunguka na kusema kuwa hakuna hata mfanyakazi mmoja wa kaunti yake ambaye amepokea mshahara wa mwezi Julai.

Mbunge wa Nambale, Bw John Sakwa Bunyasi naye aliwasihi wabunge wenzake kumaliza utata kuhusu mgao wa fedha kwa kaunti 47.

“Hizi ni pesa za umma na si za magavana. Naomba tugawe fedha hizi kwa ajili ya miradi ya maendeleo,” akasema Bw Bunyasi alipohudhuria hafla ya umma mjini Vihiga.

Katibu wa KNUN tawi la Vihiga Caleb Maloba alisema wauguzi wamepoteza motisha ya kufanya kazi na wako tayari kuandaa mgomo kudai haki yao.

“Hatutaendelea na mazungumzo yoyote. Tumekuwa na subira ilhali wanachama wetu wanaumia. Iwapo hawatakuwa wamelipa, tutaanza mgomo wetu,” akasema Bw Maloba.