Hofu ulevi ukitumbukiza wakazi 3,000 wa mtaa mmoja katika matatizo ya akili
ULIMWENGU unapoadhimisha wiki ya Afya ya Akili Duniani, viongozi katika mtaa wa mabanda wa Matisi mjini Kitale, Kaunti ya Trans Nzoia, wameungana kuangazia afya ya akili inayoathiri wakazi zaidi ya 3,000.
Visa hivi vimehusishwa na ongezeko la matumizi ya pombe haramu na mihadarati hasa miraa.
Viongozi wa eneo hilo wameungana na shirika la kijamii maarufu kama M-Shadow kufanya uhamasishaji na kuwapa msaada wahasiriwa wa afya ya kijamii.
Manaibu wa machifu eneo hilo waliacha kuwakamata wahasiriwa baada ya kugundua kufanya hivyo kunawaathiri zaidi.
“Eneo hili lina idadi kubwa ya watu na wakazi wengi wana changamoto za afya ya akili kutokana na pombe haramu na aina nyingine ya mihadarati,” alisema Chifu Mkuu eneo hilo, Janet Wafula Nekesa.
“Takwimu zetu zinaonyesha takriban watu 3,000 ni wana matatizo ya afya ya kiakili kutokana na pombe haramu.”
Alifichua kuwa unywaji wa pombe haramu umechangia ongezeko la boma kusambaratika na dhuluma za kinyumbani.
Baada ya kugundua mchakato wa kisheria haufanikiwi kuangamiza maovu hayo, amegeukia mpango wa M-Shadow unaowezesha wahasiriwa kuanza matibabu na wauzaji kushiriki aina mbadala ya kupata riziki.
“Shirika hili limetusaidia sana kupunguza visa hivi na tunatumai kuwa afya ya akili na matumizi ya pombe na dawa za kulevya yataangamizwa kupitia kampeni hii na kuwahamasisha wakazi,” alisema.
Mzee wa kijiji, Judith Nekesa aliyekuwa muuzaji wa pombe haramu anakiri kuwa maisha yake yalikuwa yamevurugika.
“Mimi sasa ni mzee wa kijiji Matisi lakini mbeleni nilikuwa muuzaji sugu wa chang’aa. Maisha yangu hayakuwa na mpangilio hadi nilipojiunga na safari ya kubadilisha tabia na kisha kuteuliwa kuwa mzee wa kijiji,” anaeleza.
Muasisi wa M-Shadow, Nancy Wamalwa, aliwasihi wanaume wanaopambana na uraibu wa mihadarati na matatizo ya afya ya kiakili kujisajili katika mpango huo ili kupata matibabu.
Licha ya hatua na maendeleo yaliyofanikishwa katika uhamasisho kuhusu afya ya akili, tafiti na matibabu, Bi Wamalwa anasema mengi yanahitajika kufanywa ili kuwasaidia wahasiriwa.