• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
Hofu wafugaji ngamia wakivamia vijiji Kwale

Hofu wafugaji ngamia wakivamia vijiji Kwale

Na FADHILI FREDRICK

MZOZO unanukia baina ya wakazi na wafugaji wa ngamia katika vijiji vya Chanzou, Makamini na Bofu Wadi ya Samburu Chengoni, eneobunge la Kinango, baada ya kuvamia mashamba ya wenyeji na kulisha mifugo yao.

Wakazi hao wamesema zaidi ya ngamia 150 na wafugaji watano kutoka eneo la Kaskazini Mashariki walivamia mashamba yao wakitafuta lishe na maji kutokana na ukame katika sehemu zao.? Baadhi ya wakazi waliokerwa na tukio hilo walionya kuchukua sheria mikononi mwao iwapo serikali itashindwa kuchukua hatua za haraka kuzima uhasama na ugomvi unaoweza kuzuka.

Akizungumza na Taifa Leo katika mahojiano ya simu, mkazi wa Chanzou, Bw Chiberya Mboga, alisema wafugaji hao wamekuwa wakilisha mifugo yao kwa mashamba ya wenyeji bila idhini kwa muda wa wiki mbili sasa.

“Hatuwezi kuendelea na shughuli zetu za kila siku kama kawaida kwa sababu ya uvamizi wa mashamba yetu na wafugaji hao haramu,” alisema.? Bw Mboga alisema vyanzo vya maji katika bwawa la Chanzou na Gozani yanakauka haraka kutokana na idadi kubwa ya mifugo ikichangiwa zaidi na ngamia hivyo basi kulazimishwa kutumia maji hayo na mifugo.

“Tunalazimishwa kutumia maji na ngamia na kuna hatari ya kuchipuka kwa maradhi na kuhatarisha afya yetu. Tumepoteza mifugo yetu kwa sababu vinyesi na mikojo ya ngamia ni sumu kwa mifugo wetu wanapokunywa maji,” akasema.

Mkazi mwingine, Bw Karani Mwayawa, alisema mifugo hiyo imeacha ardhi zao kuwa kame zaidi kwani maeneo ya malisho yamekuwa haba.

“Sasa kumekuwa na ukame sana na vyanzo vingine vya maji vinakauka pia na uwepo wa ngamia unazidisha hali ya wasiwasi ambapo kwa wenyeji hatutavumilia,” akasema.? Bw Mwayawa amewataka maafisa wa usalama kuingilia kati kabla ya mzozo kuzuka katika eneo hilo.

“Tunahofia usalama wetu na tunaomba maafisa wa usalama kusuluhisha shida hii kabla ya isababishe mapigano,” akasema Bw Mwayawa.? Vile vile, mkazi mwingine kutoka Chanzou, Bw Mwambaji Mangale, alisema wafugaji haramu wamekuwa wakihangaisha wenyeji kutafuta maji na lishe.

Alidai wafugaji hao haramu waondolewe haraka iwezekanavyo na kupelekwa walikotoka.

“Ngamia hazihifadhi chochote katika mashamba yetu zinafanya hali ya chakula kuwa mbaya zaidi. Tunaomba maafisa wa usalama kukabiliana na hali hiyo na kurejesha utulivu,” akasema.

Hata hivyo, Naibu Kamshna wa Kinango, Bw Kialo Kaloki aliwataka wakazi kuwa na subira na kuwaonya dhidi ya kuchukua sheria mikononi mwao.? “Tunaomba utulivu wakati tunatafuta suluhu ya mzozo huo,” akasema.

You can share this post!

Wauzaji vitabu walia wanapata hasara

Madaktari waonya dhidi ya dawa za kupunguza maumivu ya uke

adminleo