Habari Mseto

Hoteli motoni kwa kuzuia mwanamke kunyonyesha

May 14th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

WANAWAKE jijini Nairobi, wanatarajiwa kuandamana kesho kufuatia ripoti kwamba mama mmoja alifurushwa kutoka hotelini kwa sababu ya kumnyonyesha mtoto.

Kundi la Pregnant and Nursing Mums Kenya, limesisitiza kuwa litaongoza maandamano hayo licha ya wasimamizi wa hoteli ya Olives iliyoko barabara ya Accra, katikati ya jiji kusema haijapokea malalamishi yoyote kuhusu kisa hicho.

Kulingana na Bi Wanjeri Nderi, anayeshirikisha maandamano hayo, visa vya wanawake kudhulumiwa kwa sababu ya kunyonyesha vimeongezeka nchini.

“Hii sio mara ya kwanza wanawake wanaonyonyesha kunyanyaswa wakiwa maeneo ya umma. Wamefukuzwa au kukatazwa kunyonyesha wakiwa katika benki na mashirika mengine,” Bi Wanjeri aliambia tovuti ya NairobiNews.

Alisema wanawake wataandamana kutoka Freedom Corner hadi hoteli ya Olives kuonyesha ghadhabu zao.

Mwanamke aliyetambuliwa kama Betty Kim, 26, alidai kwenye Facebook kwamba alifukuzwa na wahudumu wa hoteli hiyo mnamo Mei 7 kwa kumnyonyesha mtoto wake. Wanawake walikasirishwa na tukio hilo wakilitaja kama dhuluma na dharau kwa wanawake.

Hata hivyo, hoteli hiyo iliwataka wanawake na wateja wake kuwa watulivu ikisema inaendelea kufanya uchunguzi ili kutatua suala hilo.

Kwenye taarifa, hoteli hiyo ilisema kuwa ilifahamu tukio hilo kupitia mitandao ya kijamii na kumtaka mama aliyetoa madai hayo kujitokeza kuwasilisha malalamiko rasmi.

Ilisema kwamba ina haki zake kama biashara ikiwa ni pamoja na kupatiwa nafasi ya kuchukua hatua za kinidhamu kwa wafanyakazi waliohusika iwapo mwanamke huyo atawasilisha malalamiko yake rasmi.

Mwanamke huyo alidai kwamba wahudumu wa hoteli hiyo walimkabili alipoanza kumnyonyesha mtoto japo alikuwa akisubiri chakula alichoagiza.

“Nilikuwa nikisubiri chakula wakati mhudumu mwanamke aliponikabili kwa dharau na kuniambia niache kumnyonyesha mtoto au nijifunike,” mwanamke huyo alisema.

Alisema alishangaa kwa sababu haikuwa mara yake ya kwanza kufanya hivyo na ulikuwa wakati wa mvua.

Mhudumu mwingine alimwendea na kumwambia kwamba alikuwa akifanya kitendo kisichofaa na alipomuuliza alikofaa kwenda kumnyonyeshea mtoto, alimwelekeza chooni. “ Alipofanya hivyo, nilihisi kudharauliwa na nikaacha kumnyonyesha mtoto,” alieleza.

Kulingana na bango lililosambazwa kwenye mitandao, maandamano yataanza Freedom Corner kupitia barabara ya Parliament hadi Olive Restaurant.