Huenda Rotich na Bett wakashtakiwa kuhusu sukari
Na CHARLES WASONGA
WABUNGE kutoka eneo la magharibi mwa Kenya kunakokuzwa miwa kwa wingi Jumanne walitoa stakabadhi ambazo huenda zikatumiwa kumfungulia mashtaka Waziri wa Fedha Henry Rotich na hatimaye kupigwa kalamu.
Viongozi hao; Ayub Savula (Lugari), Justus Murunga (Matungu) na Tindi Mwale, waliwaonyesha wanahabari stakabadhi walizodai kuwa halali kutoka afisi za serikali, zinazoonyesha jinsi Bw Rotich alidharau msimamo wa Mamlaka ya Ukusanyaji wa Ushuru Nchini (KRA) na kuruhusu kampuni 14 kuingiza sukari nchini bila kulipia ushuru.
Stakabadhi hizo zinafichua kuwa mnamo Septemba 12, 2018, aliyekuwa Waziri wa Kilimo Willy Bett alimwandikia barua Bw Rotich akimtaka kuruhusu kampuni hizo kutotozwa ushuru wa kima cha Sh10.6 bilioni.
Hii ni licha ya sukari kufika Bandarini Mombasa baada ya Agosti 31, 2018 ambayo ilikuwa ni siku ya mwisho kwa iliwekwa na Bw Rotich mwenye kwa wafanyabiashara mbalimbali kuingiza sukati nchini bila kulipia ushuri. Kipindi hicho kilianza mnamo Mei 12, 2018.
“Stakabadhi hizi kutoka kwa Wizara ya Kilimo na ile ya fedha zinaonyesha kuwa, kutokana na hatua ya Rotich, serikali ilipoteza mabilioni ya fedha baada Rotich kuruhusu uingizwaji wa tano 71,040 za sukari bila kulipiwa ushuru,” akasema Bw Savula.
Wabunge hao walisema hatua hiyo ilipelekea kutolewa kwa sukari nyingi ya bei rahisi katika soko la humu nchini na kufifisha sekta miwa nchini, inayotegemewa na wakazi wengi wa magharibi mwa Kenya.
Kwa hivyo, wabunge hao walimtaka Rais Uhuru Kenyatta kumwachisha kazi Waziri Rotich na Bw Bett ambaye mapema mwaka huu aliteuliwa balozi wa Kenya India, ;a sivyo wawafungulie mashtaka kwa kosa la uhalifu wa kiuchumi
“Tumempa Rais Kenyatta makataa ya siku saba awaachishe kazi Rotich na Bett kama kweli amejitolea kupambana na jinamizi la ufisadi. Asipofanya hivyo, sisi kama wabunge wanaowakilisha wakulima wa miwa wanaoteseka kutokana na kero la uagizaji sukari kutoka nje, “akasema Bw Murunga.
Wabunge hao walisema watawasilisha stakabadhi hizo kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na Afisi ya Idara ya Upelelezi wa Jinai ili Rotich, Bett na wakurugenzi wa kampuni husika wachukuliwe hatua za kisheria.
Aidha, waliahidi kuwasilisha stakabadhi hizo kwa Kamati ya Pamoja ya Bunge kuhusu Kilimo na Biashara inayochunguza sakata ya sukari ya magendo.
Kampuni ambazo wabunge hao wanadai zilikwepa kulipa ushuru ni; Flora Baker Limited, Piccadilly Holding Ltd, Landmark Freight Services Ltd, Pillarmatta Ltd, Option Two Limited, Ifox Commodity Ltd, Paleah Stores Ltd na Mapping Trading Company.
Zingine ni; Sukari Investment Ltd, Elon Commodity (K) Ltd, Coast Terminal East Africa Ltd, Zack Petroleum Ltd na Export Trading Company Ltd.