• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
Huzuni 3 wakifariki baada ya kufunikwa na mawe timboni

Huzuni 3 wakifariki baada ya kufunikwa na mawe timboni

ALEX NJERU na ISABEL GITHAE

WATU watatu waliaga dunia na mmoja kujeruhiwa vibaya, baada ya timbo walimokuwa wakichimba mawe kuboromoka na kuwazika Jumanne asubuhi.

Hata hivyo, watu wengine watatu waliokuwa mbali kidogo na eneo la timbo la Mutonga lililoko kwenye mpaka wa Kaunti ya Meru na Tharaka Nithi, waliepuka mauti baada ya kutoroka wakati mkasa huo ulipotokea.

Walioshuhudia walisema kuwa wanne hao walikuwa wakichonga mawe katika sehemu ya chini kabisa ya timbo wakati ukuta wa mawe wa urefu wa takriban mita kumi ulibomoka na kuwaangukia.

“Ilikuwa mwendo wa saa nne wakati ukuta wa mawe kutoka sehemu ya juu ulibomoka na kuwazika watu hao kabisa,” akasema Charles Kithuka ambaye alishuhudia.

Maafisa kutoka shirika la Msalaba Mwekundu wakishirikiana na polisi, kikosi cha uokoaji cha kaunti na wanakijiji walisaidiana na kuondoa miili iliyokuwa imezikwa na mawe wakitumia tingatinga, kisha wakapelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya Meru Level Five.

Naibu Kamishna eneo la Imenti Kusini Mugo Gichiri, alisema kuwa kazi katika kware hiyo ambayo iko katika sehemu ya barabara ilikuwa imesimamishwa na Mamlaka ya Kusimamia Mazingira nchini (NEMA), baada ya kuibuka kuwa kulikuwa na hatari kwa waliokuwa wakifanya kazi pale na wapita njia.

Alisema kuwa mmiliki wa timbo hilo atawajibika kufuatia mkasa huo na kugharimikia vifo vilivyotokea kwani alikosa kufuata maagizo ya serikali.

“Timbo hili liliharamishwa na NEMA muda mrefu uliopita na mmiliki wake amekuwa akiiendesha kinyume na sheria,” akasema Bw Gichiri.

OCPD wa eneo hilo John Cheruiyot alisema mmiliki huyo atafunguliwa mashtaka kuhusiana na vifo hivyo, kwa kuendesha timbo bila kibali, pamoja na hatia nyingine.

“Tutamkamata mmiliki wa timbo na kumshtaki kortini,” akasema.

Kutokana na mkasa huo, shirika la msalaba mwekundu sasa limewataka wafanyakazi katika timbo kutoingia kazini hadi wakati msimu wa mvua utaisha.

Imeripotiwa kuwa visa hivyo vimekuwa vikijitokeza kila mara msimu wa mvua unapoanza au kuendelea kwa kipindi fulani.

You can share this post!

Mtoto afariki baada ya kamba aliyochezea kukwama shingoni

ODM kuwania urais 2022 bila kuwajali vinara wa Nasa

adminleo