Habari Mseto

Ibada iliyoangusha kampuni za kamari za Betin, SportPesa

December 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na PAUL WAFULA

MASAIBU ya kampuni ya SportPesa na kampuni nyingine za uchezaji kamari yalianza Mei mwaka uliopita, baada ya ibada moja ya kanisa iliyohudhuriwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Kwenye hafla hiyo, iliyofanyika katika kanisa la Christ is the Answer Ministries (CITAM), Nairobi, aliyekuwa kiongozi wa kanisa hilo, Askofu Mstaafu David Oginde, alishangaa ni kwa nini Rais Kenyatta alikuwa akiongoza nchi iliyozongwa na uchezaji kamari.

Baada ya ibada hiyo, Rais Kenyatta alikutana na Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, ambapo alimtaka kuchunguza na kumweleza yaliyokuwa yakiendelea katika sekta ya uchezaji kamari nchini.

Baada ya muda, Dkt Matiang’i alirejea kwa Rais Kenyatta, akiwa na maelezo ya kutamausha kuhusu hali ilivyokuwa ikiendelea nchini.

Miongoni mwa maelezo hayo ni kwamba, vifo vya matineja nchini vilikuwa vikiongezeka kila kuchao.

Vile vile, ilibainika kuwa zaidi ya vijana 500,000 walio kati ya umri wa miaka 18 na 25 walikuwa wameadhibiwa na Halmashauri ya Kudhibiti Ulipaji Mikopo (CRB) kwa kushindwa kulipa mikopo waliyokuwa wamekopa kama ada za uchezaji kamari.

Kwenye ufichuzi huo, Shirika la Watengenezaji Bidhaa Kenya (KAM) lililalamika kwamba matumizi ya baadhi ya bidhaa muhimu yalikuwa yakipungua.

Wakuu wa vyuo vikuu pia walilalamika kuwa wanafunzi wengi hawakuwa wakihudhuria masomo yao, kwani walikuwa wakitumia muda wao mwingi katika uchezaji kamari.

Cha kushtua ni kuwa, walipohudhuria, walikuwa wakitumia muda wao mwingi kwenye simu zao wakishiriki kwenye uraibu huo.

Dkt Matiang’i pia alieleza kuwa kiwastani, mapato ya washiriki wengi yalikuwa kati ya Sh5,000 na Sh10,000 kwa mwezi. Baada ya hali hiyo kuibuka, waziri alimwagiza Inspekta Jenerali wa Polisi Hilary Mutyambai kufanya uchunguzi kwa muda wa saa 24 kuhusu wakurugenzi wa kampuni hizo. Alisema alikuwa tayari kutia saini stakabadhi za kuwarejesha makwao mara moja.

Kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo’, Dkt Matiang’i alisema alilazimika kuchukua hatua hiyo ili kulainisha hali kwenye sekta hiyo.

Miongoni mwa wakurugenzi waliofurushwa nchini ni Bw Domenico Giovando na mwanawe, Leandro Giovando. Wawili hao walikuwa wakurugenzi wa kampuni ya Betin.

Vile vile, alimfurusha Bw Nikolai Barnwell, ambaye alikuwa mkurugenzi wa kampuni ya BetPawa. Watatu hao ni raia wa Bulgaria.