ICC yapuuzilia mbali madai ya Ruto
Na WALTER MENYA
MAHAKAMA ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC), imekana madai ya Naibu Rais William Ruto kwamba kuna njama ya kufufua kesi dhidi yake katika chombo hicho.
Kwenye mahojiano yaliyochapishwa katika gazeti la ‘Daily Nation’ Ijumaa, Naibu Rais alidai kuwa wale ambao walipanga njama ya kuwazuia kuingia mamlakani mnamo 2013 sasa wanapanga kumzuia kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.
“Mwaka jana nilipokuwa nikizungumza na mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS) Philip Kameru, niligundua kuwa kuna watu ambao wanataka kufungua upya kesi za ICC,” alisema Dkt Ruto.
Lakini Jumamosi, Afisi ya Kiongozi wa Mashtaka katika mahakama ya ICC ilikana madai hayo.
“Afisi ya Kiongozi wa Mashtaka haiwezi kutoa kauli yoyote,” ikasema taarifa ya aya tatu kwa maswala ambayo ‘Taifa Jumapili’ iliona.
Katika taarifa hiyo, afisi ya kiongozi wa mashtaka ilisema kuwa licha ya kwamba mashtaka dhidi yao kuondolewa, bado milango i wazi na mashtaka yanaweza kufunguliwa ikiwa ushahidi mpya utapatikana.
Lakini afisi hiyo haikuweza kufichua ikiwa kuna ushahidi wowote ambao unaweza kupelekwa kuchunguzwa upya au kufufuliwa kwa kesi dhidi ya Dkt Ruto.
“Kama mnavyofahamu mnamo Aprili 5, 2016, mahakama iliondoa mashtaka dhidi ya William Samoei Ruto na Joshua Arap Sang’ lakini ikasema wazi kuwa itafufua kesi endapo kutapatikana ushahidi mpya,” taarifa hiyo ikasema.
Ikaongeza: “Kulingana na Kipengee cha 15 cha Sheria za Roma zilizobuniwa mahakama ya ICC, mtu yeyote au kundi la watu kutoka popote duniani anaweza kutuma habari kuhusu makosa kwa kiongozi wa mashtaka. Na afisi hiyo ina wajibu wa kuweka siri habari zozote itakazopokea. Afisi hii huchambua inavyohitajika kulingana na Sheria za Roma bila mapendeleo.”
Kwenye ripoti yake katika shirika la Umoja wa Mataifa mwaka wa 2018, ICC ilisema kwamba uchunguzi kuhusu kesi za Kenya ungali unaendelea licha ya kutamatishwa kwa kesi hizo.
Hakuna mwandani wa Dkt Ruto aliyekuwa na habari kuhusu madai hayo. Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen alisema hakuwa na habari kuhusu uchunguzi dhidi ya Naibu Rais.