Idadi ya waliopona Covid-19 nchini Kenya yafika 1,164
Na SAMMY WAWERU
KATIKA kipindi cha saa 24 zilizopita watu 72 wamepona ugonjwa wa Covid-19, idadi jumla ya waliothibitishwa kupona ugonjwa huu kabisa nchini ikifika 1,164
Akiridhia habari hizi njema, Waziri Msaidizi wa Afya Dkt Rashid Aman amesema Ijumaa kuwa kuthibitishwa kupona kwa idadi ya juu ya wagonjwa kama hiyo kunasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa katika vituo vya afya.
“Hizi ni habari nzuri kwetu kuona wagonjwa wanapona kwa sababu hali hii inatusaidia kuhudumia visa vipya vya maambukizi,” Dkt Aman ameambia wanahabari katika Ukumbi wa KICC, Nairobi.
Hata hivyo, Waziri amesema vita dhidi ya Covid-19, janga ambalo sasa ni kero ya ulimwengu mzima, vitashinda ikiwa Wakenya watazingatia mikakati na masharti yaliyotolewa kudhibiti maambukizi.
Mikakati hiyo ni pamoja na kunawa mikono kila wakati, kuzingatia umbali kati ya mtu na mwingine, kuvalia barakoa katika maeneo ya umma, kuepuka mazingira yanayoshuhudia misongamano ya watu na pia kusalia nyumbani ikiwa mtu hana shughuli zozote za umuhimu mkubwa maeneo ya umma.
Katika muda wa saa 24 zilizopita, Kenya imethibitisha visa vipya 90 vya maambukizi ya virusi vya corona, idadi jumla ya wagonjwa ikigonga 3,305
Dkt Aman amesema visa hivyo vimethibitishwa kutoka kwa sampuli 2,419 zilizokusanywa, kukaguliwa na kufanyiwa vipimo. Aidha, kufikia sasa Kenya imepima jumla ya sampuli 108,666.
Maambukizi mapya ya Ijumaa, visa vyote ni raia wa Kenya, 62 wakiwa wanaume na 28 wanawake. Mgonjwa mdogo ana umri wa miaka 14, huku wa juu akiwa na umri wa miaka 80.
Dkt Aman ametuma salamu za pole kwa familia za wagonjwa wanne ambao wameangamizwa na Covid-19, idadi jumla ya waliofariki kutokana na ugonjwa huu sasa ikifika watu 96 nchini.