Idara yaomba mabilioni kujenga nyumba 500,000 za bei nafuu
Na BERNARDINE MUTANU
SERIKALI imeombwa kutoa Sh6 bilioni za ujenzi wa nyumba 500,000 za gharama ya chini.
Idara ya Ujenzi imeomba Bunge kuidhinisha fedha hizo kwa lengo la kufanikisha ajenda ya serikali ya maendeleo.
Kulingana na idara hiyo, Sh2 bilioni zitakuwa za ujenzi wa nyumba hizo na zingine Sh4 bilioni zitakuwa za kuimarisha mitaa duni.
Kulingana na Katibu Mkuu Aidah Munano, idara hiyo inalenga kuanzisha hazina ya kufadhili ujenzi wa nyumba na kufanya marekebisho Shirika la Kitaifa la Ujenzi (NHS).
Kulingana na katibu wa nyumba Bw Patrick Bucha, ujenzi wa nyumba katika mtaa wa mabanda wa Kibera Mariguini, Soweto “B” na Kiambiu unahitaji Sh14.4 bilioni ingawa nyumba za gharama ya chini zitagharimu Sh4 bilioni katika ujenzi wake.
Kulingana naye, Hazina ya Kitaifa ilikuwa imeipa idara hiyo Sh3 bilioni ambazo hazikutosha.
“Ili kutimiza ajenda ya rais, tunahitaji takriban Sh6 bilioni,” alisema Bw Bucha. Idara hiyo inaendelea kujenga nyumba za bei ya chini Mavoko, Shauri Moyo, Parklands na Makongeni lakini kwa majaribio tu.