IEBC kuwahoji 10 kwa wadhifa wa afisa mkuu
Na BENSON MATHEKA
TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeorodhesha watu 10 watakaohojiwa kujaza wadhifa wa Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo.
Wadhifa huo uliachwa wazi baada ya Ezra Chiloba kutimuliwa kufuatia tofuati zake kali na mwenyekiti wa tume hiyo, Wafula Chebukati na ukiuakaji wa kanuni za ununuzi.
Kwenye tangazo katika vyombo vya habari Alhamisi, IEBC ilisema ilipokea maombi kutoka kwa Wakenya 97 kati ya Mei 21 na Juni 3 2019, muda ambao ilikuwa imetoa wa kutuma maombi.
Ilisema kwamba, ilipokea maombi kutoka kwa watu wawili baada ya muda huo kukamilika na kuchagua kumi ambao watahojiwa kati ya Juni 24 na 26 mwaka 2019.
Miongoni mwa waliochaguliwa ni Bw Marijan Marjan Hussein ambaye amekuwa akishikilia wadhifa huo tangu Bw Chiloba aliposimamishwa kazi kabla ya kufutwa rasmi.
Wengine watakaohojiwa ni Dkt Mabonga Joel Lusweti kutoka Bungoma, Bw Naktari Okuku Humprey kutoka Busia, Bw Aura Zephania Okeyo kutoka Homabay na Mhandisi Kioko Paul Christopher Kimali kutoka Kitui.
Wanawake
Bi Nancy Wanjiku Kariuki, Dkt Elishiba Muthoni Murigi na Bi Anne Kerubo Mwasi ni wanawake wa pekee katika orodha hiyo.
Wanaume wengine katika orodha ya watu kumi ni Dkt Benjamin Tarus Kipchumba na Dkt Khalid Billow.
Mnamo 2016, Bw Aura alikuwa wa kwanza kwenye mahojiano ya kutafuta Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo akiwa na alama 80 lakini wadhifa huo ukapatiwa Bw Chiloba.
Kulingana na taarifa ya IEBC, Bw Aura atahojiwa Juni 24 mwaka huu.
Bw Chiloba alisimamishwa kazi Aprili mwaka jana ili kutoa nafasi ya uchunguzi kuhusu ununuzi wa vifaa vilivyotumiwa kwenye uchaguzi wa 2017.
Kusimamishwa kwake kulisababisha mgawanyiko katika tume na makamishna watatu waliokuwa wakimtetea Paul Kurgat, Margaret Mwachanya na Connie Maina wakajiuzulu.
Mnamo Jumanne, Bw Chebukati alisema shughuli za tume hazikuathiriwa na ukosefu wa Afisa Mkuu Mtendaji.
Kulingana na mwenyekiti huyo, tume ilikuwa na kaimu afisa mtendaji ambaye ni Marjan Marjan Hussein.