Habari MsetoSiasa

Inasikitisha serikali kuchelewesha fedha kwa maeneo kame – Mbunge

March 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Kilifi Kaskazini Owen Baya, ameilaumu serikali kwa kuchelewesha usambazaji wa pesa za Hazina ya Kusawazisha Maendeleo (Equalization Fund) katika kaunti 14 zilizoko nyuma kimaendeleo nchini.

Akiongea katika kamati ya bunge kuhusu fedha na mipango, Bw Baya alisema kwa miaka tisa iliyopita serikali ya kitaifa imewasilisha Sh1.1 bilioni, pekee kati ya jumla ya Sh12.4 bilioni kwa kaunti 14 zilizotambuliwa kuwa nyuma kimaendeleo.

Kwa mujibu wa kipengee 204 cha Katiba pesa za hazina hiyo zinapasa kutumika kufadhili miradi ya maji, afya, umeme na barabara.

“Inasikitisha kuwa Wizara ya Fedha imekwamilia pesa hizi miaka tisa baada ya katiba hii kuanza kutumika huku maeneo lengwa kama kama kaunti yangu ya Kilifi yakizongwa na changamoto. Sh763.5 milioni ambazo wizara inasema zilipelekwa katika kaunti ya Kilifi mwaka huu wa kifedha zilitolewa mnamo 2016,” akasema katika majengo ya bunge, Nairobi.

“Na miradi iliyoanzishwa na fedha hizo sasa imekwama,” Bw Baya akaongeza.

Mbunge huyo alisema alipokuwa akijibu taarifa kutoka kwa Waziri Msaidizi wa Fedha Bw Nelson Gaichuhie ambaye alisema wizara yake haijasambaza pesa hizo kwa sababu wabunge hawajapitisha sera itakayowezesha idara za serikali kutambua miradi ya kufadhiliwa.