Habari Mseto

IPOA yachunguza kisa cha OCS kuuma sikio raia

August 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na KALUME KAZUNGU

HALMASHAURI ya Usimamizi wa Huduma na Utendakazi wa Polisi nchini (IPOA) imeanzisha uchunguzi kwa kisa ambapo OCS anayesimamia kituo cha Polisi cha Bandari ya Lamu (LAPSSET), alimvamia mwanamke mmoja na kumuuma hadi kumkata sikio lake la kushoto.

Kupitia ujumbe wake kwa vyombo vya habari, Mwenyekiti wa IPOA, Bi Anne Makori alisema waliafikia kuchunguza tukio hilo baada ya kupokea malalamishi yaliyowasilishwa na mmoja wa raia kuhusiana na kudhulumiwa kwa mwanamke huyo, Bi Racheal Mwaura,34.

Kisa hicho kilitokea katika eneo linalokaribiana na kituo hicho cha polisi eneo la Kililana mnamo Agosti 20.

Aidha malalamishi yaliwasilishwa kwa IPOA mnamo Agosti 23, siku tatu baada ya kitendo hicho kufanyika.

Bi Mwaura pia aliumizwa mkono wake wa kulia wakati wa uvamizi uliotekelezwa na naibu huyo wa OCS ambaye baadaye anadaiwa kutoweka.

IPOA ilisema tayari imetuma maafisa wake kuchunguza tukio hilo na kuahidi kwamba itatekeleza haki kwa mdhulumiwa iwapo afisa huyo atapatikana na hatia kuhusiana na tukio hilo.

“Ningependa kuthibitisha kwamba IPOA imepokea malalamishi ya kudhulumiwa kwa Bi Racheal Mwaura, 34 na Naibu wa OCS wa kituo cha LAPSSET. Wakati wa uvamizi huo, Bi Mwaura alikatwa sikio lake na kisha kujeruhiwa mkono wake. Alikuwa akiendeleza shughuli zake eneo hilo wakati OCS alipomvamia na kumpiga. Tumetuma maafisa wa kitengo chetu maalum ili kulichunguza,” alisema.

Katika mahojiano na Taifa Leo, mamake mwaathiriwa, Bi Teresia Mwaura alikashifu vikali kitendo hicho cha kinyama kilichotekelezwa na afisa huyo wa polisi na kuiomba serikali kutekeleza uchunguzi wa haraka ili haki itendeke kwa msichana wake.

“Mwanangu ndiye anayetegemewa katika familia yetu. Sasa amesababishiwa majeraha na afisa wa polisi ambaye alifaa kumlinda. Ningeomba uchunguzi wa haraka ufanywe ili mwanangu apate haki. Alidhulumiwa,” akasema Bi Teresia.

Kwa upande wake, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia alithibitisha tukio hilo na kusema kuwa uchunguzi wa kina tayari unaendelezwa na polisi.

“Ni kweli kisa kilitendeka na tayari polisi wanaendeleza uchunghuzi wa kina juu ya tukio hilo. Si vyema kwa afisa wa polisi anayefaa kulinda raia kugeuka na kuwa adui kwa wananchi. Akipatikana na hatia ataadhibiwa,” akasema Bw Macharia.

Aidha juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Lamu, Muchangi Kioi ili kuzungumzia suala hilo na pia kuthibitisha iwapo afisa husika amekamatwa au la ziligonga mwamba kwani simu yake haikupokelewa alipopigiwa.