Jaguar afichua sababu ya kukamatwa kwake
Na CHARLES WASONGA
MBUNGE wa Starehe Charles Njagua Kanyi amethibitisha kuwa amekamatwa na anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Nairobi Area.
Kupitia ujumbe kwenye akaunti ya Twitter Bw Kanyi, maarufu kama Jaguar, amesema anashuku kuwa alikamatwa kuhusiana na madai kuwa aliwachochea wachuuzi waliokuwa wakilalamikia ugavi usio wa haki wa vibanda katika soko jipya la Mwariro.
“Wakati huu niko Nairobi Area (kituo cha polisi). Sielewe kosa langu lakini ninashuku kukamatwa kwangu kunahusiana na mzozo kuhusu ugavi wa vibanda vya soko la Mwariro,” amesema.
Mbunge huyo wa Jubilee amesisitiza ataendelea kutetea kile alichodai ni ugavi usio wa haki wa vyumba vya kibiashara katika soko hilo jipya.
Jaguar alimakatwa saa chache baada ya Mshirikishi wa Nairobi Wilson Njenga kuwaonya wanasiasa dhidi ya kuwachochea wafanyabiashara kuhusiana na suala hilo.
Amesema kamati maalum imeteuliwa kuongoza mchakato wa ugavi wa nafasi za kufanyia biashara kwa wafanyabiashara halali na waliosajiliwa.
Kamati hiyo, Bw Njenga akasema, inaongozwa na Kamishna wa Kaunti ya Nairobi Flora Mworia.
“Kuna watu ambao wamekuwa wakizunguka wakikusanya pesa kwa kisingizio cha kuwatengea wafanyabiashara nafasi katika soko hili. Nawataka wafanyabiashara kutulia kwani nimeteua kamati maalum itakayosimamia ugavi wa haki wa vibanda vya shughuli za biashara katika soko la Mwariro,” akasema Bw Njenga.
Afisa huyo amewahakikishia wafanyabiashara katika masoko mapya yaliyoko maeneo ya Gikomba, Westlands na Karandini (Dagoreti Kusini) kwamba ugavi wa maeneo ya shughuli za kiuchumi utaendeshwa kwa haki.
“Mpango huo ukiendelea, polisi wanaendelea kuchunguza wanasiasa ambao walichochea vurugu katika soko la Mwariro Ijumaa wiki jana,” akasema Bw Njenga.