Habari MsetoSiasa

Jamii ya Waluo yamsifu Tuju

November 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na DICKENS WASONGA

VIONGOZI wa jamii ya Waluo wamemmiminia sifa Katibu Mkuu wa Chama cha Jubilee, Bw Raphael Tuju na kusema amesaidia sana jamii hiyo akiwa serikalini.

Seneta wa Siaya, Bw James Orengo alisema Bw Tuju ambaye ni waziri asiyesimamia wizara yoyote mahususi, amekuwa akiwasaidia sana viongozi wa eneo hilo ingawa hakusema ni msaada aina gani.

Bw Tuju (pichani) alikuwa hasimu mkubwa katika jamii hiyo tangu alipoungana na Rais Mstaafu Mwai Kibaki katika kuunga mkono marekebisho ya katiba mwaka wa 2005.

Hata hivyo, hali imebadilika tangu Rais Uhuru Kenyatta alipoweka muafaka wa maelewano na Kiongozi wa ODM Raila Odinga mwaka wa 2018 na Bw Tuju ameonekana kuwa mshirika wa karibu mno na Bw Odinga.

“Yale ambayo Bw Orengo amesema hapa ni ya kweli. Nafurahi hakusema zaidi na pia mimi sitasema zaidi ya yale aliyoyasema. Ninajua huwa tunapenda kujadili kila kitu hadharani lakini lazima tujifunze kuweka mambo mengine siri,” akasema.

Viongozi hao walizungumza wakati wa mazishi ya Mama Loice Anyango ambaye ni mke wa mpiganiaji uhuru marehemu Achieng Oneko, katika kijiji cha Kunya, eneobunge la Rarieda mnamo Jumamosi.

Bw Tuju alirejelea msimamo wake kwamba hana nia kuwania ugavana katika Kaunti ya Siaya, akisema macho yake yamelenga nyadhifa za serikali kuu.

Wanaotarajia kupambania ugavana wa Siaya 2022 ni Bw Orengo, Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi na aliyekuwa Mbunge wa Rarieda Nicholas Gumbo.