Jaribio la Kiunjuri kuagiza mahindi ugenini lazimwa
Na CHARLES WASONGA
KAMATI ya Bunge kuhusu Kilimo imepinga pendekezo la Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri kwamba pana haja ya serikali kuagiza mahindi kutoka nje ikisema kuna mahindi ya kutosha nchini.
Wanachama wa kamati hiyo jana walisema kuna takribani magunia milioni nne ya mahindi nchini ambayo yanatosha kukidhi hitaji la kitaifa hadi Septemba msimu wa mavuno utakapoanza rasmi.
“Uchunguzi wetu umebaini kuwa, kuna jumla ya magunia 2.6 milioni ya mahindi katika maghala ya Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB). Kando na hayo, wakulima na wasagaji unga bado wanashikilia jumla ya magunia 1.5 milioni ambayo kwa jumla, yanatosheleza mahitaji yetu hadi Septemba,” mwenyekiti wa kamati hiyo Adan Haji (Mandera Kusini) akawaambia wanahabari katika katika majengo ya bunge.
Bw Haji aliongeza kwamba wakulima wa mahindi katika maeneo ya South Rift na Magharibi mwa Kenya tayari wameanza kuvuna ishara kwamba maeneo hayo hayatakumbwa na uhaba wa bidhaa hiyo kuanzia mwezi ujao.
Naye naibu mwenyekiti wa kamati hiyo Bw Emmanuel Wangwe (Navakholo) alisema wazo la Bw Kiunjuri linalenga kuwafaidi wafanyabiashara walaghai wala sio wakulima wa taifa hili haswa wale wenye mashamba madogo.
“Hamna haja yoyote kwa Wizara ya Kilimo kuagiza mahindi kwa bei ya Sh4,000 kwenda juu ilhali juzi ilishindwa kununua mahindi ya wakulima wetu kwa angalau Sh3,000. Tunapinga kabisa hatua kama hii wakati ambapo hamna uhaba wa mahindi,” akasema.
Mbw Haji na Wangwe walikuwa wameandamana na wanachama wengine wa kamati hiyo; Justus Murunga (Matungu), Silvanus Osoro (Mugirango Kusini) na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake, Busia Florence Mutua.
Wiki jana, Waziri Kiunjuri alipendekeza kuwa ipo haja ya kuagizwa kwa magunia 19.5 milioni ya mahindi kutoka ng’ambo kutokana na uhaba wa bidhaa hiyo nchini.
Kulingana na waziri huyo magunia 12.5 milioni yatatumiwa kuzalisha unga wa matumizi ya binadamu huku magunia 6 milioni yakitumiwa kutengeneza lishe ya mifugo.
Bw Kiunjuri alisema hatua hiyo ndio itasaidia kupunguza bei ya unga wa mahindi ambao umepanda hadi kufikia Sh125 kwa paketi moja ya kilo mbili mwezi huu kutoka Sh80 Januari.
Pendekezo hilo pia limepingwa na mwenyekiti wa Bodi ya Kusimamia Hazina ya Mahindi ya Kimkakati (SGRB) Dkt Noah Wekesa na wabunge kadhaa kutoka eneo la North Rift kunakozwa mahindi kwa wingi.
Dkt Wekesa alishikilia kuwa kuna mahindi ya kutosha nchini na hamna haya ya kuagiza mengine kutoka nje
Wakiongea na habari jana katika majengo ya bunge, wanachama wa kamati hiyo walisema kuna takriban magunia milioni nne nchini yanatosha.