Jeshi la KDF halitatoka Somalia – Mwathethe
Na WACHIRA MWANGI
Wanajeshi wa Kenya hawataondoka Somalia hadi nchi hiyo iwe huru kutokana na mashambulio ya Al-Shabaab, Mkuu wa Majeshi Meja Jenerali Samsom Mwathethe amesema.
Mkuu wa Majeshi aliyekuwa akizungumza alipotembelea wanajeshi wa Kenya katika eneo la Kudhey nchini Somalia, Jumamosi, alisema KDF walitumwa nchini humo kwa ajili ya usalama wa Kenya.
“Serikali ya Kenya ilituma majeshi yake nchini Somalia kwa sababu tunaamini tukiangamiza Al-Shabaab nchi itakuwa salama,” akasema.
“Ni heri tukabiliane na adui huku Somalia ili tuishi kwa amani bila wasiwasi nchini Kenya,” akaongezea.
Alisema kuwa japo wanajeshi wa KDF wako chini ya usimamizi wa vikosi vya Umoja wa Afrika (Amisom), Kenya ina malengo yake ya kibinafsi; kuhakikisha kuwa Al-Shabaab wanaangamizwa ili ukanda huu uwe na amani ya kudumu.
Meja Jenerali Mwathethe alisema kuwa alifurahishwa na ripoti ya kutia moyo aliyopewa na Kamanda wa KDF katika eneo la Kudhey, Erick Lovega.
“Nimefurahishwa kuwa nanyi leo. Nilianza safari yangu wiki iliyopita kuanzia Makao Makuu ya Jeshi na kisha nikatembelea wanajeshi wa Angani jijini Nairobi. Baadaye, nilielekea katika Makao Makuu ya Wanajeshi wa Majini jijini Mombasa.
Akaendelea: “Imepita miaka minane tangu mlipokuja hapa. Kulikuwa na changamoto za hapa na pale lakini mmekuwa wakakamavu na mmeweza kumlemea adui.”
Meja Mwathethe alisema kuwa serikali ya Kenya imejitolea kuhakikisha kuwa wanajeshi wa KDF wanatumia silaha za kisasa katika kukabiliana na magaidi wa Al-Shabaab.
“Tumewapa vifaa vya kisasa na nina imani kwamba kambi ya Kudhey haitashambuliwa na magaidi. Mmepewa silaha za kisasa nanyi pia ni wakakamavu,” akasema.
Meja Jenerali aliyewasilisha salamu za Krismasi kutoka kwa Amri Jeshi Mkuu, Rais Uhuru Kenyatta, aliwataka wanajeshi wa KDF kuwa macho wakati huu wa msimu wa sherehe.
“Nawahimiza kuhakikisha kwamba Al-Shabaab hawafiki karibu na eneo lenu la ulinzi. Wakenya wanawatakia heri mnapokabiliana na adui,” akasema.
“Napenda kuwafahamisha kwamba hatujawasahau. Mmefanya maisha ya wakazi wa eneo hili kuwa bora. Watoto wao sasa wanaenda shule bila uoga,” akasema.
Mkuu wa Majeshi alikuwa ameandamana na Kamanda wa Majeshi ya Majini Meja Jenerali Levy Mghalu, Mkurugenzi wa Ujasusi Jeshini Brigedia Said Mohammed Farah, Mkuu wa Operesheni za Kijeshi kati ya maafisa wengineo.