‘Jicho Pevu’ azua msisimko kwa ufasaha wa lugha bungeni
Na CHARLES WASONGA
MBUNGE wa Nyali, Mohamed Ali Jumatano aliwachangamsha Wabunge wenzake kwa kutumia lugha sanifu ya Kiswahili alipowasilisha hoja yake kwa mara ya kwanza, hali iliyowafanya wenzake kutumia lugha hiyo ya taifa kuijadili kwa saa tatu mfululizo.
Hoja ya Bw Ali, ambayo pia iliandikwa kwa Kiswahili, inahimiza Serikali Kuu kuwezesha kuwepo kwa Hospitali ya Rufaa ya Kitaifa katika kaunti ya Mombasa kuhudumia eneo zima la Pwani.
Mbunge huyo anasema japo Sheria ya Afya ya 2017 inapendekeza kujengwa kwa hospitali za rufaa katika kila mojawapo ya kaunti 47 nchini, kuna hospitali mbili pekee za rufaa nchini hali inayofanya wengi kukosa huduma za kiafya.
Hospitali zenyewe ni; Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) iliyoko jijini Nairobi na ile ya Rufaa na Mafunzo ya Moi (MTRH) ambazo katika siku za hivi karibuni zimekuwa zikipokea idadi kubwa ya wagonjwa kutoka humu nchini na mataifa jirani.
“Na hali ni mbaya zaidi katika eneo zima la pwani lenye jumla ya kaunti sita kwani hamna hospitali hata moja ya rufaa. Ndipo kupitia hoja napendekeza kujengwe hospitali ya hadhi hiyo au ile ya Coast General ipandishwe hadhi,” akasema Bw Ali, almaarufu “Jicho Pevu” jina ya makala yake ya zamani katika runinga.
Hii, akasema, ndio njia ya kipekee ya kufanikisha hitaji la katiba linalompa kila Mkenya haki ya kupata kiwango bora cha huduma ya afya.
“Kuanzishwa kwa Hospitali ya Kitaifa ya Rufaa kutakuwa ni afueni kubwa kwa wagonjwa kutoka kaunti za Tana River, Lamu, Kilifi, Taita Taveta na Kwale ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakisaka matibabu ya kiwango cha juu katika hospitali za KNH na MTRH,” akasema Bw Ali mwanahabari wa zamani.
Bw Ali ambaye ni mwanahabari mtajika, alisema hospitali kama hiyo pia inapasa kutoa mafunzo katika taaluma ya udaktari ikizingatiwa idadi ya madaktari humu nchini ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya Wakenya.
“Taifa hili lina jumla ya madaktari 11,000 lakini ni madaktari 6,000 pekee wanaohudumu wakati huu, hali ambayo imechangiwa na baadhi yao kwenda ughaibuni kutokana na mishahara duni. Hii ndio maana taifa linahitaji madaktari zaidi na vifaa vya kiafya,” akasema
Wabunge wa pande zote mbili wakiongozwa na kiongozi wa wachache John Mbadi waliunga mkono hoja hiyo huku wakiitaka serikali ya kitaifa kutekeleza mapendekezo yake.