• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Jina langu si tiketi ya Ikulu, Ruto aambia wapinzani

Jina langu si tiketi ya Ikulu, Ruto aambia wapinzani

Na PETER MBURU

NAIBU Rais William Ruto sasa anadai viongozi wa upinzani hawana mpangilio wowote unaoweza kuwaletea ushindi wa urais ila wanatumia jina lake kiholela kupiga siasa, na wakicheza hawatawezana naye katika uchaguzi wa 2022.

Akirejelea matamshi ambayo alikuwa akitumia kabla ya uchaguzi wa 2017, Dkt Ruto jana alisema kuwa viongozi wa upinzani badala ya kukabili masuala halisi wamekuwa wakimtajataja tu akiwataka kumkoma.

Ingawa hakutaja kiongozi yeyote alipohutubu kwenye ziara yake katika Kaunti ya Wajir, Naibu Rais ambaye hasimu wake mkubwa wa kisiasa ni Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, alishauri viongozi wa upinzani wajipange upya kama kweli wanataka kushindana naye ifikapo mwaka wa 2022 kwenye uchaguzi wa urais.

“Naona wakishindwa tena. Ikiwa wanataka kushindana 2022, nawaambia Ruto si mradi, yeye si sera, wala si mradi wa maendeleo. Ruto ni jina la mtu,” akasema Dkt Ruto, alipokuwa katika hafla ya kuzindua miradi Kaunti ya Wajir, kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na afisi yake ya mawasiliano.

Naibu Rais alikuwa akizungumzia wakazi, katika hafla ambapo alikuwa ameandamana na viongozi 15 wa Jubilee, akiwemo kiongozi wa wengi bungeni Aden Duale.

Matamshi yake yalitokea siku moja tu baada ya mkutano uliokuwa umepangiwa kufanyika Kakamega ulioandaliwa na wandani wa Bw Odinga kutibuka katika hali ya kutatanisha.

Mkutano huo ambao ajenda yake ilisemekana kuwa kutoa msimamo mmoja kuhusu vita dhidi ya ufisadi, ambavyo Dkt Ruto na wandani wake wamekuwa wakidai vinafanywa kwa njia ya kumwandama kisiasa, ulifutiliwa mbali dakika za mwisho.

You can share this post!

‘Team Komboa Kenya’ yajitokeza kukabili...

Serikali yaelekeza macho Amerika kusaka wafadhili

adminleo