Jinsi basi la Al-Mukaram lilivyogonga trela saa saba usiku na kuua abiria 10
WATU 10 wamefariki na wengine 26 kujeruhiwa baada ya basi lililokuwa likisafiri kutoka Mandera kugonga trela lililokwama eneo la Bangal kwenye barabara ya Garissa-Mwingi.
Abiria wanane walifariki papo hapo huku wengine wawili wakifariki katika Hospitali ya Rufaa ya Garissa walipokuwa wakipokea matibabu.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Bangale Ephraim Karimi alisema basi hilo kutoka Mandera lilikuwa na zaidi ya abiria 50.
Mkuu huyo wa polisi alisema mtoto wa miaka minne alikuwa miongoni mwa waliofariki, huku Mohamed Abdi, 5, akinusurika lakini alimpoteza mamake kwenye ajali hiyo.
Abiria wengine kumi wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Garissa.
“Mwendo wa saa saba na nusu usiku basi moja kutoka Mandera hadi Nairobi lilihusika katika ajali eneo la Katumba kuelekea Mwingi, inasikitisha kwamba tulipoteza watu wanane papo hapo,” akasema Bw Karimi.
Alisema basi hilo linaloitwa la Al-Mukaram, liligonga trela iliyokwama.
“Trela hilo lilikuwa lilikuwa limeharibika na kuegeshwa kando ya barabara. Inaonekana dereva wa basi hilo alikuwa akiendesha mwendo wa kasi wakati wa ajali hiyo,” alisema Bw Karimi.
Dereva, ambaye alinusurika na majeraha, atatoa taarifa kwa polisi pindi atakapoondoka hospitalini, Bw Karimi alisema.
Miili katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Garissa imetambuliwa tangu wakati huo na Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya lilikuwa katika harakati za kuwasiliana na familia za waathiriwa.
“Ajali hiyo ilikuwa ya kusikitisha na bado sijajua hasa kilichotokea. Gari lilikuwa katika hali nzuri,” alisema Bw Bardad Mohamed, mmiliki wa kampuni ya basi ya Al-Mukaram.
Kampuni hiyo inasifika kwa kubadilisha jina la mabasi yake kila yanapopata ajali ili kuepuka kulipa fidia kwa abiria.
Ilianza kama Tawakali kabla ya kuhamia Makka, na baada ya mauaji ya walimu mwaka 2014 na watu walioshukiwa kuwa Al-Shabaab na ajali nyinginezo, ilibadilisha jina na kuwa Al-Mukaram.
Abiria wengi walikuwa wamepanda basi hilo katika miji ya Mandera, Rhamu na Elwak.
Msimamizi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Garissa Mahat Salah alisema kituo hicho kilipokea miili minane kutoka eneo la tukio na manusura kumi na watatu waliojeruhiwa vibaya.
“Tulipoteza wawili ambao walikuwa katika hali mbaya,” alisema.