• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Jinsi kikundi kinavyosaidia jamii wakati huu wa janga la Covid-19

Jinsi kikundi kinavyosaidia jamii wakati huu wa janga la Covid-19

Na MAGDALENE WANJA

KIKUNDI cha vijana chini ya shirika la World Leaders of Today kimekuwa katika mstari wa mbele katika kusaidia jamii zisizojiweza katika kukabiliana na janga la Covid-19.

Shirika hilo lisilo la serikali pia ni la kimataifa na limekuwa katika mstari wa mbele katika kunyunyuzia dawa ya kuua viini kuepuka maambukizi ya corona, kutoa mafunzo kwa jamii na kutoa msaada wa chakula.

Mwanzilishi wa shirika hilo Bw Peter Moll alisema wiki jana kuwa mara nyingi na hasa wakati huu wa janga la corona, vijana wengi wamekuwa wakijihusisha na uhuni na matumizi ya dawa za kulevya ila kikundi hiki cha vijana kinajihusisha katika kusaidia jamii.

Bw Moll alisema kuwa huduma hizo wanazitoa kwa kuzingatia masharti na sheria zilizowekwa na serikali ili kuzuia maambukizi.

“Tangu kuzinduliwa kwa mradi huu, tumeweza kuzisaidia jamii 513 ambazo ni sawa na watu 3,000. Hii ni pamoja na wanafunzi 94 ambao ni watahiniwa ambapo tuliwapa vifaa muhimu katika masomo,” alisema Bw Moll.

Huduma hii pia inasaidia familia 2,800 katika kuwasaidia walimu, wazazi, vijana na viongozi wa kijamii ambao husaidia katika usambazaji wa msaada.

Baadhi ya wanachama wa kikundi cha vijana chini ya shirika la World Leaders of Today. Picha/ Magdalene Wanja

Kati ya mitaa duni ambayo imefaidika sana kutokana na mradi huu ni ule wa Kibera.

Bw Moll aliongeza kuwa mradi huu sasa unaenezwa katika kaunti zingine zikiwemo Siaya, Kirinyaga, Narok, Kisumu, Trans Nzoia, Kitui, Nakuru, na Laikipia.

You can share this post!

Naivas yawapa wahudumu wa afya wa Thika Level 5 vyakula na...

Ni rasmi Gor Mahia itawakilisha Kenya katika CAF Champions...

adminleo