Habari Mseto

Jinsi ya kutambua dhehebu lenye imani potovu

March 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA MHARIRI

WAUMINI huhitajika uaminifu wao wote uwe kwa kiongozi wao wa kidini, na hii huhitaji kukatiza mahusiano ya kifamilia na kirafiki ama kubadilisha taaluma na mambo mengine uliyokuwa ukifanya.

Waumini sugu wanahisi hawawezi kuishi nje ya kundi na huogopa kuacha kundi kwa hofu ya kufuatwa na mikosi wakiamua kuacha imani.

Ukosoaji wa imani ama kiongozi hukemewa sana na wakati mwingine wanaofanya hivyo huadhibiwa.

Mbinu za kuvuruga akili kama vile taamuli, kusifia mfululizo na kuongea kwa ndimi zinatumika kupindukia kwa nia ya kuondoa shaka kuhusu kiongozi ama kundi husika.

Kiongozi hutoa masharti kuhusu jinsi wafuasi wake wanavyofaa kufikiria na kuishi. Mfano ni wafuasi kuomba ruhusa kutoka kwa kiongozi kabla ya kuanza mahusiano ya kimapenzi, kubadilisha kazi, kuoa, ama kiongozi anawaambia aina ya mavazi wanayofaa kuvaa miongoni mwa masharti mengine.

Kundi hujiona kuwa limo katika hadhi ya juu kuliko imani zingine, na kiongozi wao wanamwona kuwa mtu maalum mwenye jukumu la kuokoa binadamu, na hupewa majina makubwa makubwa ya kidini.

Wafuasi huwaona watu wengine wasiofuata imani yao kama waliopotoka na wachafu.

Kiongozi huwa hawajibiki kwa yeyote. Ndiye mwenye usemi wa mwisho.

Kundi hutoa mafunzo ambayo si ya kawaida. Kwa mfano waumini kuambiwa kufanya mambo ambayo kwa kawaida yanaonekana kukiuka mitindo na maadili, ambayo kama si imani hiyo hawangefanya.