Habari Mseto

Joho awaonya vijana wanaohangaisha wakazi Mombasa

July 31st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

 

Na WINNIE ATIENO

GAVANA wa Mombasa Hassan Joho amefichua jinsi baadhi ya vijana wanavyowahangaisha wakazi hususan wafanyabiashara katika jiji hilo.

Bw Joho alisema vijana hao wanavamia wafanyibiashara wakiwalazimisha walipe fedha ili waruhusiwe kuendeleza shugli zao.

Aidha aliwasihi maafisa wa polisi kuwatia mbaroni vijana hao na kuwafungulia mashtaka.

Alisema vijana wengi wanaojihusisha na uhalifu huo wamo sehemu za Shelly Beach wilayani Likoni.

“Huo ufuo wa Shelly si wa mtu binafsi bali ni mali ya umma. Wale wanaofanya biashara zao waruhusiwe. Lakini kuna baadhi ya vijana ambao wanajaribu kuzua vurugu. Kama wewe ni mmoja wa wale ambao wanawakataza wafanyabiashara dhidi ya kuendeleza shughuli zao ukilazimisha ulipwe, tunakuangalia kwa makini,” alisema Bw Joho.

Gavana huyo amewataka wafanyabiashara hao kusimama kidete dhidi ya dhuluma hizo.

Alisema ufuo huo utalindwa dhidi ya vijana wenye tabia hiyo akisisitiza kuwa chuma chao ki motoni.

“Tunamsihi afisa mkuu wa polisi kushika doria na kuwamakata vijana hao wahalifu. Kijana yeyote ambaye anahangaisha na kuwadhulumu wachuuzi wetu anafaa kuchukuliwa hatua kali za kisheria. Wakamatwe na polisi na kupelekwa mahakamani kujibu mashtaka dhidi yao. Hatuwezi kukubali uhalifu huu uendelee; wanadhania wanaweza kuvunja sheria na wasichukuliwe hatua zozote,” alisisitiza akisema sheria itachukua mkondo wake.

Baadhi ya wafanyabiashara hao walisema huwa wanalipa fedha au la sivyo watahangaishwa.