Habari MsetoSiasa

Joho awapa polisi maski kusambazia umma

April 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

DIANA MUTHEU na MOHAMED AHMED

GAVANA wa Mombasa, Bw Hassan Joho ametoa msaada wa barakoa kwa maafisa wa polisi ili wazipeane kwa wananchi wasiokuwa nazo, badala ya kuwakamata.

Haya yalijiri baada ya gavana huyo kupokea chakula cha msaada mnamo Jumatano kutoka kwa Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai.

Akizungumza katika ofisi yake, Gavana Joho alimwomba Bw Mutyambai kuwaelekeza maafisa wa polisi wawape barakoa wananchi watakaopatikana wakitembea au kusafiri bila kujikinga, badala ya kuwanyaka.

“Tumepata bandali nne ya unga kutoka kwa Idara ya Polisi ambazo tumepewa na Inspekta Jenerali. Kwa upande wetu, tunakupa barakoa uwape maafisa wako na zingine zaidi zipewe wananchi katika vizuizi vya polisi,” akasema Bw Joho.

Bw Joho alimwomba Bw Mutyambai kuwaelekeza maafisa wake kuchukua barakoa hizo katika ofisi zake.

“Tumekubaliana na Inspekta Jenerali kuwa watu watakaopita katika vizuizi watapewa barakoa hizo. Hata hivyo, ni onyo kwa watu wote kuwa lazima wavae maski hizo baada ya kuzipata au la sivyo, sheria itachukua mkondo wake,” akasema.

Ombi la gavana huyo linakuja siku moja baada ya Bw Mutyambai kutangaza kuwa wananchi watakaopatikana bila barakoa hizo watakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Hii ni baada ya Wizara ya Afya kutangaza kuwa mtu yeyote atakayepatikana bila barakoa atatozwa faini ya Sh20,000 au kifungo cha hadi miezi sita.

Bw Mutyambai alikubali ombi la gavana huyo akisema, “Namshukuru Gavana Joho kwa kutupa barakoa za kutosha kwa maafisa wa polisi. Tumekubaliana maafisa hao watatotoa zingine kwa wananchi.”

Alisema kuwa agizo la kila mtu kuvalia kifaa hicho ni moja ya hatua ya kuzuia ueneaji wa virusi vya corona.

“Tunaelewa kuwa si kila mmoja anaweza kupata pesa za kununua barakoa lakini polisi watatoa msaada wao. Pia ni vizuri tufuate maagizo kwa kuzivalia,” akasema.