Jumwa hatarini, achunguzwa kwa kumumunya mamilioni
Na JOHN KAMAU
MBUNGE wa Malindi, Bi Aisha Jumwa amejikuta katika shida zaidi baada ya wapelelezi kugundua mamilioni ya pesa za Hazina ya Serikali Kuu ya Kustawisha Maeneobunge (NG-CDF) na za Serikali ya Kaunti ya Kilifi zilitumwa kwa akaunti zake za kibinafsi.
Imebainika kwamba akaunti za benki za Bi Jumwa zilianza kushukiwa Juni 2019 na Kituo cha Kuchunguza Fedha ambacho ni shirika la serikali linalosaidia kuchunguza na kufuatilia matumizi ya pesa za kiuhalifu.
Uchunguzi wao ulipata mamilioni ya pesa ziliingizwa kwa akaunti hizo kwa njia zilizotiliwa shaka. Mkurugenzi wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) George Kinoti alithibitisha wanaendeleza uchunguzi huu.
Hayo yamefichuka wakati ambapo Bi Jumwa tayari anachunguzwa kwa kifo cha Jola Ngumbao aliyepigwa risasi wakati mbunge huyo alipovamia boma la Bw Reuben Mwambire Katana, ambaye alikuwa mgombeaji udiwani wa ODM katika uchaguzi mdogo wa Wadi ya Ganda.
Aliachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000 pesa taslimu pamoja na msaidizi wake, Bw Geoffrey Okuto.
Taifa Leo haingethibitisha kwa njia huru ikiwa pesa alizotumiwa zilikuwa za biashara halali, lakini Sheria ya Maadili ya Maafisa wa Umma inasema kwamba, “afisa wa umma hatatumia mamlaka yake vibaya kujitajirisha, kutajirisha mume au mkewe, shirika, wala kitengo chochote ambacho anahusika nacho.”
Jana, Bi Jumwa alipuuzilia mbali upelelezi huo na kusema ni kisingizio kwani yeye ni maskini sana hata anatafuta pesa.
“Mimi hutoka Ganze na nimefilisika sana. Sifahamu kuhusu habari hizi, ni propaganda tupu. Sina pesa. Natafuta pesa,” akasema.
Kwa muda mrefu mwaka huu, mbunge huyo amejitokeza kimasomaso kuwa mwandani mkubwa wa Naibu Rais William Ruto kwa kiwango cha kukosana na viongozi wa chama chake cha ODM.
Hivi majuzi, aliwalaumu Gavana wa Kilifi Amason Kingi na mwenzake wa Mombasa Hassan Joho kwa masaibu yanayomkumba. Wawili hao ni washirika wa karibu wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.
Uchunguzi unaoendelezwa umelenga makampuni manne ambayo yalitumiwa kutuma pesa hadi katika akaunti za Bi Jumwa.
Makampuni hayo ni Bizcot Limited inayosimamiwa na Bw Okuto (msaidizi wa Jumwa) ambayo mkurugenzi wake mwingine ni Bw Joseph Otieno.
Mengine ni Kaseru Construction Limited ambayo wakurugenzi wake ni Karisa Kalume na Selina Kalume, walio mwana na binti wa Jumwa mtawalia. Kampuni nyingine ni Multiserve Contractors Limited ambayo wakurugenzi wake ni Robert Katana Wanje na Rachel Neema Karisa, mkaza mwana wake.
Upelelezi huo ni miongoni mwa nyingine zinazoendelezwa nchini kote kuhusu jinsi wanasiasa hutumia makampuni kujifaidi kwa pesa za NG-CDF na zabuni zinazotoka katika serikali za kaunti.
Stakabadhi zilionyesha kwamba kati ya Novemba 2017 na Desemba 2018, Multiserve ilipokea Sh19 milioni kutoka kwa NG-CDF ya Malindi na Sh48.4 kutoka Kaunti ya Kilifi.
Sh2.5 milioni zilitumwa baadaye kwa akaunti ya kibinafsi ya Bi Jumwa mnamo Septemba 12, 2018, kisha akatuma Sh2.8 milioni kutoka kwa akaunti yake hadi kwa kampuni ya ujenzi kujenga jumba la vyumba vinne vya kulala Nairobi.