Habari Mseto

Jumwa matatani kwa kushambulia viongozi Pwani

December 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MOHAMED AHMED

MBUNGE wa Malindi Aisha Jumwa kwa mara nyingine amejipata matatani akikashifiwa kwa kuwamiminia matusi viongozi wa Pwani wakiwemo magavana Amason Kingi wa Kilifi na mwenzake wa Mombasa Hassan Joho kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa Msambweni.

Bi Jumwa amekuwa akiwakashifu viongozi hao wakati wa mikutano ya kampeni ambayo amekuwa akimpigia debe mgombea wa kujitegemea Feisal Bader anayeungwa mkono na Naibu Rais Dkt William Ruto.

Kwenye mikutano mingi, Bi Jumwa amekuwa akiwarejelea Mabw Joho na Kingi kama magavana wazembe na kudai hawajatekeleza chochote cha maana tangu wachaguliwe mnamo 2013.

“Hamfai kuwa na wasiwasi kuhusu Gavana Kingi. Hana chochote yule na hatabadilisha chochote hapa Msambweni. Ametutia aibu sana sisi wakazi wa Kilifi kwa kuwa amekuwa mtu wa mkono wa Bw Joho. Anafuata tu Bw Joho na hawezi kumpinga kamwe,” alisema Bi Jumwa kwenye mkutano moja wa kisiasa.

Mnamo Jumamosi, viongozi kutoka Kaunti ya Kilifi walimkemea Bi Jumwa kwa kuwa na mazoea ya kuwatusi viongozi wa ODM, wakisema alikuwa akifanya hivyo kumridhisha Naibu Rais Dkt William Ruto.

Bw Kingi naye alimkashifu Bi Jumwa akimwambia hakuchaguliwa na wakazi wa Malindi kuwatusi viongozi wengine bali kuwakilisha bungeni.

“Ulichaguliwa kutuwakilisha bungeni lakini umekuwa kimya sana wala huchangii mijadala. Unafaa ukome kuendelea kututia aibu sisi wakazi wa Malindi,” akasema Bw Kingi wakati wa mazishi ya mkewe diwani wa Dabaso.

Mbunge Mwakilishi wa kike wa Kilifi Getrude Mbeya naye alimshutumu Bi Jumwa akisema amekuwa na tabia ya kuwatusi viongozi wasiokuwa na msimamo sawa naye kisiasa hasa Mabw Kingi na Joho.

“Kila moja wetu ametusiwa na Bi Jumwa na tumechoka. Tafadhali Bw Kingi tupe mwelekeo kama mzee wetu wa kisiasa. Tuunganishe kabla uondoke mamlakani mnamo 2022,” akasema Bi Mbeyu.

Mbunge wa Magarini Michael Kingi naye alikuwa wazi akisema kuwa Bi Jumwa amekuwa akiwatusi viongozi wanaounga mkono ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI).

“Nimetusiwa kwangu Magarini mara nyingi na Bi Jumwa ambaye huja na kuwaambia watu jinsi mbunge wao ni ovyo. Alikuwa mbunge mwakilishi wa kike na hakuna chochote cha maana alichofanya. Amegundua kwamba upinzani wake kwa ripoti ya BBI hautampa maarufu wowote hapa na sasa amegeukia matusi,” akasema Bw Kingi.

Mbunge huyo alionya mwenzake wa Kilifi Kaskazini Owen Baya kwa kuendeleza ushirikiano na Bi Jumwa ambaye alimlinganisha na Dellilah mwanamke katika bibilia aliyemhadaa Samsoni.

Naibu Waziri wa Ardhi Gideon Mung’aro ambaye alikuwa mbunge wa zamani wa Kilifi alimtaja Bi Jumwa na wanaopinga BBI kuwa maadui wa raia. Bw Mung’aro alisema kuwa BBI inawahusu raia na wale wanaoikataa hawataki watu wanufaike.

“Kwa mfano hapa Kilifi tutapata maeneobunge mengine hapa Kilifi. Gavana atakayeingia kuanzia 2022 atapata pesa zaidi na wanaopinga ripoti hiyo wanahofia kipengele kinachosema wafisadi lazima kesi zao zikamilike kwa muda wa miaka mbili,” akasema.

Bi Jumwa amekuwa mshirika mkubwa wa Gavana wa Kwale Salim Mvurya ambaye pia yupo mrengo wa Naibu Rais Dkt Ruto hasa wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Msambweni unaofanyika kesho.