Kabogo bado amwandama Waititu, afufua kesi ya vyeti
Na JOSEPH WANGUI
ALIYEKUWA Gavana wa Kaunti ya Kiambu, William Kabogo, amefufua kesi ambayo alitilia shaka vyeti vya masomo vya mrithi wake Ferdinand Waititu.
Licha ya Waititu kuondolewa mamlakani baada ya kushtakiwa kwa ufisadi, Bw Kabogo alifahamisha mahakama kwamba anataka kuendelea na kesi hiyo.
Bw Kabogo, kupitia kwa wakili Issa Mansour, amekata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu wa kutupilia mbali kesi yake mnamo 2016.
Amefufua kesi hiyo katika rufaa inayosikilizwa na Majaji Asike Makhandia, Fatuma Sichale na Jamila Mohammed.
Mnamo Ijumaa, majaji hao walimuuliza Bw Kabogo iwapo anataka kuendelea na kesi hiyo hata baada ya ushindani wa kisiasa kati yake na Bw Waititu kutulia na Bw Mansour akasema masuala yaliyo katika kesi hiyo ni muhimu na ya kisheria.
Majaji hao walimwagiza Bw Kabogo kumkabidhi Bw Waititu ilani ya kesi kabla ya kutenga tarehe ya kuisikiliza.
Katika rufaa yake, Bw Kabogo anataka majaji wasimamishe uamuzi wa Jaji Joseph Onguto wa Mahakama Kuu aliyesema kwamba korti haikuwa na mamlaka ya kusikiliza na kuamua madai aliyozua kumhusu Waititu.
Jaji Onguto alimwagiza Kabogo kulipa Waititu Sh5.3 milioni kama gharama ya kesi.
Bw Kabogo alikuwa amedai kwamba digrii ya Bw Waititu kutoka Chuo Kikuu cha Punjab nchini India ilikuwa feki na hakuhitimu kushikilia wadhifa wa umma. Aidha, alitaka Mahakama kuamua kwamba “Ferdinand Ndung’u Waititu ni tofauti na Clifford Ndung’u Waititu”.
Bw Kabogo alisema alikuwa na habari kwamba mnamo Januari 11, 2013, Waititu alikuwa ameapa kuwa ndiye Clifford Ndung’u Waititu aliyefanya mtihani wa darasa la saba (CPE) katika Shule ya Msingi ya Mbagathi mwaka wa 1975.
“Kwa mujibu wa sheria kuapa uongo ni sawa na kuiba jina. Kitendo kama hicho ni tabia ya uhalifu iliyo na adhabu katika sheria za uhalifu na inakiuka sehemu ya 13 ya sheria za uongozi na maadili,” aliambia mahakama.
Lakini kwenye uamuzi wake, Jaji Onguto alisema suala hilo linafaa kushughulikiwa na Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi (EACC).
Alisema mahakama isingechunguza vyeti vya masomo vya Bw Waititu.
Bw Waititu aliondolewa mamlakani na madiwani wa bunge la kaunti ya Kiambu na Naibu Wake James Nyoro akaapishwa kuwa gavana.