• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
KAFYU: Familia zadai haki baada ya kujeruhiwa na polisi

KAFYU: Familia zadai haki baada ya kujeruhiwa na polisi

NA KALUME KAZUNGU

FAMILIA mbili, Kaunti ya Lamu zinadai haki kutendeka kwa watu wao waliopigwa na kuacha na majeraha mabaya na polisi waliokuwa wakishika doria wakati wa kafyu.

Familia ya Bw Said Mohamed Omar,31 kutoka kijiji cha Matondoni, Kaunti Ndogo ya Lamu Magharibi na ile ya Bi Nyasumani Suleiman,27 kutoka kijiji cha Kizingitini, Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki zimekashifu maafisa wa polisi waliowavamia vijana wao wakiwa ndani ya nyumba zao, ambapo waliwapiga bila huruma na kuwaacha na majeraha mabaya wakidai wanashinikiza kuheshimiwa kwa amri ya kafyu kwenye maeneo hayo.

Bw Omar anadai alikuwa akitazama filamu ndani ya nyumba yake kijijini Matondoni majira ya saa mbili kasorobo usiku kabla ya maafisa wa polisi wapatao 40 kuingia ghafla ndani ya nyumba yake kupitia mlango uliokuwa wazi na kuanza kumpiga kwa viboko, makofi na mateka.

Anasema wakati wa tukio hilo, polisi walimuumiza vibaya kwenye mbavu, kifua na hata nyonga yake, hatua ambayo imepelekea yeye kulazwa kwenye hospitali ya King Fahad mjini Lamu.

Bw Omar anasema wakati wa tukio hilo, polisi pia waliharibu viti vyake ndani ya nyumba hiyo kabla ya kwenda zao.

“Mimi nilikuwa ndani ya nyumba yangu nikifuatilia filamu huku mlango nikiwa nimeuacha wazi. Waliingia ghafla na kudai wanatafuta watu ambao wamekuwa wakikaidi amri ya kafyu. Walianza kunipiga bila huruma na kuvunjavunja viti vyangu. Baadaye walibeba Sh 12,000 zilizokuwa ndani ya nyumba yangu na kwenda nazo. Kabla ya kutoweka, pia walihangaisha majirani kwa kuwasukumasukuma,” akasema Bw Omar.

Mama wa mwaathiriwa, Bi Fathiya Abdallah, aliomba serikali kujitokeza na kueleza wazi kwa nini maafisa wa polisi kuwadhulumu raia wasiokuwa na hatia.

“Sijafurahishwa na tendo la polisi la kumpiga mwanangu ambaye alikuwa kajituliza nyumbani mwake. Hakuwa amekaidi amri ya kafyu. Kwa nini walimpiga na alikuwa ndani ya nyumba yake? Ombi langi ni mwanangu apate haki,” akasema Bi Abdallah.

Kijijini Kizingitini, Bi Nyasumani Suleiman alisema polisi wapatao watatu waliingia ndani ya nyumba yao na kuanza kuwavurumisha makonde na mateke majira ya saa moja unusu.

Bi Nyasumani anasema nguo aliyokuwa amevaa kwa wakati huo iliraruliwa na maafisa hao wa usalama kabla ya kuwapiga wanafamilia watatu na kisha kuondoka.

“Walinipiga mimi na watu wengine watatu wa familia yetu kabla ya kutoweka. Tunadai haki itendeke kwani tulikuwa kwa nyumba yetu. Hatukuwa tumekosea mtu wala kuvunja amri ya kafyu,” akasema Bi Nyasumani.

Shirika la kutetea haki za binadamu kwa waislamu (MUHURI) lilikashifu kitendo hicho cha polisi cha kukiuka haki za binadamu.

“Yeyote akivunja sheria lazima sheria hiyo hiyo ifuatwe kwa kushikwa na kushtakiwa. Kumpiga mshukiwa si jambo jema. Tunalaani kitendo hicho cha maafisa wa usalama na tunafuatilia ili kuona kwamba mdhulumiwa anapata haki,” akasema Afisa Mkuu wa Muhuri, tawi la Lamu, Bi Umulkher Salim.

Kwa upande wake aidha, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia alisema ofisi yake bado haijapokea malalamishi yeyote kutoka kwa umma kwamba polisi walikuwa wakipiga watu masaa ya kafyu.

“Mimi sijapokea ripoti au malalamishi yoyote ya watu kupigwa kiholela na polisi wakati wa kafyu eneo hili. Ninafuatilia. Cha msingi ni watu kuheshimu kafyu na wakae majumbani mwao,” akasema Bw Macharia.

You can share this post!

Vijana Samburu wahamasisha jamii kuhusu corona

Jinsi Kenya inavyoweza kuimarisha viwanda vyake

adminleo