Habari Mseto

KAFYU: Msongamano Likoni wapunguzwa

March 29th, 2020 1 min read

NA WACHIRA MWANGI NA FAUSTINE NGILA

MAGARI sasa yanaruhusiwa kuvuka kivuko cha Likoni kuanzia saa tano asubuhi na saa tisa alasiri ili kuwapa waabiri kwa feri nafasi kuvuka bila bughudha, Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho amesema.

Maamuzi hayo yalifikiwa katika mkutano wa gavana, wabunge na mratibu wa eneo hilo John Elungata kufuatia vimbwanga vya Ijumaa ambayo ilikuwa siku ya kwanza ya kafyu, kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Gavana Joho aliamuru kuwa waabiri wapewe kipaumbele kuanzia Jumamosi, ili kupunguza kukaribiana kwa watu.

“Tunawaomba wananchi na washika doria wakumbuke kuwa sisi sote tuko katika kafyu na tutafaulu iwapo tutazingatia maagizo,” alisema.

Magari yatazuiliwa ili abiria wawe na wakati mwafaka wa kuvuka. Wakazi wataruhusiwa kuvuka kuanzia saa kumi na mbili asubuhi hadi saa tano mchana na saa tisa hadi saa kumi na mbili jioni ili wawe na wakati murua wa kufika nyumbani kabla ya kafyu.

Seneta wa Mombasa Mohamed Faki alikemea utumiaji wa nguvu kupita kiasi uliotekelezwa na polisi kwa wananchi.

“Feri ni huduma muhimu kwa wananchi wa Mombasa. Watu wengi hutumia feri na ni lazima kuwe na msongamano. Tunaomba serikali kutuelewa. Kuwaadhibu wananchi na kuwatupia vitoa machozi kutaharibu kazi nzuri yenye inaendelea hapa,” Seneta Faki alisema.

Aliomba kuundwe kamati maalum ya wanaotumia feri ili kusimamia abiria.

“Maamuzi mengi tuliofikia hapa hayajahusisha wananchi,” alisema.

Aliwaomba waajiri wawe wanaruhusu wafanyakazi wao kufunga kazi alasiri ili waweze kutii sheria ya kafyu.