Kagwe akaangwa kuwatishia wahudumu wa afya
NA WANGU KANURI
Matamshi ya Waziri wa Afya Mutahi Kagwe yameibua hisia tata katika mtandao wa kijamii wa Twitter huku Wakenya wengi wakionekana kukerwa na aliyosema waziri huyo hapo Desemba 18.
Matamshi hayo aliyosema wakati wa kufunguliwa kwa hospitali katika Kaunti ya Muranga eneo la Kenol, yalielekezewa wahudumu wa afya ambao walikuwa wananuia kugoma kwa sababu ya kupuuzwa kwa matakwa yao.
Hii ni baada ya korti kusitisha mgomo huo wa wahudumu wa afya huku wakuu wa wahudumu wa afya wakielezwa na korti kuwa na kikao na wakuu katika wizara ya afya ili kutafuta suluhu ya malamishi ya wahudumu wa afya.
Waziri Kagwe aliwarai wahudumu wa afya kurejea kazini kwani bado ugonjwa wa Covid-19 umetukodolea macho huku akiwaomba wawe na utu na kuwasaidia wananchi. “Ninawarai mrejee kazini ili kuzuia kupoteza kazi yako. Tafadhali usiwe katika ratibu ya wanaosaka kazi mwaka ujao,” Waziri Kagwe akasema.
Wahudumu hawa wa afya wamekuwa wakiomba serikali kusikiza kilio chao kufuatia mazingira mabaya ya kazi wakati huu wa janga la Corona. Hali kadhalika, wahudumu hawa ambao wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa vifaa muhimu vya kujizuia wanapowahudumia wagonjwa, wamekuwa wakipuuziliwa huku malalamishi yao yakitupiliwa mbali.
Isitoshe, wahudumu hawa ambao wameteta kuhusu mishahara wanayopata isiyoafikiana na iliyochelewa, wameonekana kuchoshwa na ahadi tupu kutoka wizara hiyo ya afya na serikali kwa jumla huku wakisema watagoma.
Wananchi walionekana kukerwa na matamshi ya waziri Kagwe walikuwa na haya ya kusema kupitia hashtegi ya SomeoneTellKagwe:
“Azungumzie wauguzi na wahudumu wa afya na heshima,” akasema @Kinotithenurseactivist.
“Ni haki yetu kulindwa. Vifaa vya kujilinda, malipo ya bima na posho ya kutulinda dhidi ya hatari,” akaandika @TimothyBeth.
“Wauguzi wanakufa sababu ya mkurupuko wa magonjwa yanayotamba haraka sana huku wakipewa ya posho ya kutulinda dhidi ya hatari ya shilling 3850,” akasema @Stephenkeoro.
“Ni wapi vitisho vimewahi kutatua shida?” akauliza @PurityMburugu.
“Mgomo uliositishwa ulikuwa tofauti na mgomo huo ulikuwepo kwa muda wa mwezi mmoja na nusu. Mgomo wa kitaifa wa wahudumu wa afya bado unaendelea,” ukurasa wa @kUCOofficial ukasema.
“Wezi wa KEMSA wanafurahi huku madaktari wanakufa. Kumwambia daktari ahudumie mgonjwa wa Covid-19 bila vifaa vya kumkinga ni sawa na kumuua daktari huyo. Nchi yenye afya ni nchi yenye fedha. Walinde madaktari nao watawalinda wagonjwa,” akaandika @KipropDismas4.