Kahaba aliyefungwa maisha kwa mauaji ya mwenziwe aachwa huru
Na Richard Munguti
MAHAKAMA ya Rufaa Ijumaa ilimwachilia huru kahaba aliyekuwa amefungwa jela maisha kwa mauaji ya mwanamke raia wa Rwanda.
Mahakama ilikashifu polisi kwa kuzembea kuwatia nguvuni watu waliomuua mwanamke huyo ndani ya lojing’i Nairobi miaka saba iliyopita.
Majaji Martha Koome, Hannah Okwengu na Fatuma Sichale, walishutumu polisi kwa kukosa kufuata taarifa muhimu walizopewa na mpenzi wake marehemu, Bw Simon James Smith, ambaye ni raia wa Uingereza.
Marehemu Winnie Uwambaye Colpitts aliyeuliwa mnamo Februari 16, 2013 alikuwa mjamzito na alikuwa akihudumu ukahaba pamoja na Antoinette Uwineza almaarufu Micheline Uwababyyi jijini Nairobi.
Majaji hao,walisema polisi walikosa kuwahoji wanaume wawili miongoni mwao Jeane Claude, raia wa Rwanda na raia mwingine wa Congo kwa jina Collins. Korti ilielezwa kuwa Winnie aliuawa kwa kunyongwa ndani ya chumba kilichokodishwa na Jeane na Uwineza.