Habari Mseto

Kajwang’ aonja ghadhabu za madiwani

May 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

MOHAMED AHMED na IBRAHIM ORUKO

KIKAO cha Jumatano cha mkutano kati ya wawakilishi wa wadi (MCAs) na maseneta unaoendelea Mombasa, ulisambaratika baada ya Seneta wa Homa Bay, Moses Kajwang kutoa kauli ambayo iliwakasirisha washiriki.

Hii ni baada ya Seneta Kajwang kuwaambia wawakilishi hao kwamba alihitaji kuwapa mafunzo ya Kiingereza ili waelewe msimamo wake kuhusu Hazina ya Maendeleo ya Wadi.

Wawakilishi hao walihisi kudharauliwa na seneta huyo na wakamtaka kuomba radhi.

Lakini seneta huyo alikataa, hali ambayo iliwalazimisha baadhi ya wawakilishi kufika jukwaani kumwondoa kutoka ukumbini kwa nguvu.

Bw Kajwang, ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Seneti ya Uwekezaji (PIC), alikuwa mratibu wa kikao hicho baada ya washiriki kujadili kuhusu upataji wa mapato katika maeneo ya kaunti, na majukumu ya kaunti katika utoaji bora wa huduma.

Bw Kajwang’ mara kwa mara ameonekana kukataa hazina hiyo ambayo alisema haina umuhimu wowote. Wawakilishi hao walikuwa wakimtaka kuweka wazi msimamo wake kuhusu hazina hiyo.

Wakati wa mkutano na kamati simamizi za katika Kaunti ya Mombasa wiki jana, Bw Kajwang aliwaomba wenyeviti wa kamati hizo kutilia maanani umuhimu wa hazina hiyo kabla ya Seneti kujadili mswada huo ambao unatarajiwa kusomwa kwa mara ya pili katika Bunge la Seneti.

Wakati wa mkutano wa jana, aliwasifu wawakilishi hao kwa kusema walikuwa na uwezo mkubwa wa kutekeleza majukumu, hata hivyo, hakueleza wazi msimamo wake kuhusu hazina hiyo ikizingatiwa kuwa wawakilishi wa wadi wamekuwa wakishinikiza kupata fedha hizo.

Ni wakati huo ambapo kiongozi wa wengi katika Bunge la Kaunti ya Nakuru, Stanley Karanja aliposimama na kumtaka Bw Kajwang kuweka wazi msimamo wake kuhusu mswada huo.

Aliitaka Seneti pia ifutiliwe mbali ikiwa haiwezi kulinda mabunge ya kaunti.

Bw Kajwang alisema Seneti ingetilia maanani athari za mswada huo kabla ya kuanza kutekelezwa, matamshi ambayo yaliwachanganya wawakilishi hao, ambao haja yao kuu ni kwa mswada huo uungwe mkono.

“Ikiwa mnahitaji mafunzo ya Kiingereza kutofautisha maelezo na mapendekezo, hilo ni suala tunaloweza kujadili baadaye,” alisema Bw Kajwang, jambo lililofanya azomewe na wawakilishi hao waliomtaka kuondoa kauli hiyo na kuomba radhi.

Baadaye, mwandalizi wa Mswada huo, Seneta Irungu Kang’ata wa Murang’a alisema MCAs ndio wanaotangamana zaidi na wananchi na hivyo wanafahamu zaidi mahitaji yao.

Bw Kang’ata alisema wengi wa maseneta wanaunga mkono Mswada huo na kueleza matumaini kuwa utapitishwa.