• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 1:22 PM
KALRO yahimiza wakulima kukumbatia teknolojia kuimarisha uzalishaji

KALRO yahimiza wakulima kukumbatia teknolojia kuimarisha uzalishaji

Na RICHARD MAOSI 

ONYESHO la siku mbili la kilimo na teknolojia katika Kaunti ya Nakuru lilimalizika Ijumaa katika eneo la Naivasha, hafla iliyoandaliwa na Wizara ya Kilimo kwa ushirikiano na serikali ya kaunti.

Wafanyibiashara, wakulima, wanafunzi na wawakilishi wa kimataifa kutoka Uingereza, Ujerumani na Italia walimiminika kupigia debe mbinu bora za uzalishaji na vyombo mwafaka vya kuongeza mazao, wakihimiza ufaafu wa teknolojia katika kilimo.

Bw Eliud Kireger ambaye ni mkurugenzi wa shughuli za KARLO (Naivasha), aliwarai vijana kukumbatia kilimo kwani ni uti wa mgongo kwa taifa akisema ni njia nyingine ya kutengeneza nafasi zaidi za ajira na kujikomboa kutoka kwenye lindi la umaskini.

“Hatua ya Wakenya kufika hapa ni wazi kwamba kilimo kimeinua maisha yao. Tunajizatiti kuhakikisha wakulima wanafaidika na shirika letu ili kujiongezea kipato,” Kireger alisema.

Wakulima wadogo kutoka kaunti ya Nakuru, Nyandarua, Kisii, Nairobi na Machakos walionyesha kiu ya kutafuta mbinu za kukabiliana na magugu na jeshi viwavi ambalo ni tishio kwa mimea yao.

Kampuni ya Greenlight iliwakilisha mtambo wa kunyunyizia maji shambani kupitia miale ya jua,na kuwavutia watazamaji wengi katika kibanda chao cha maonyesho ya bidhaa zao.

Afisa wa mauzo wa Greenlight Planet Bw Cyrus Muchai akiwasimulia wanafunzi na wakulima namna ya kutumia miale ya jua mjini Naivasha. Picha/ Richard Maosi

Afisa wa Greenlight Cyrus Muchai aliwaelimisha watazamaji namna mkulima anaweza kuzalisha kawi kutokana na jua .

“Kwa sababu ya mfumuko wa bei ya mafuta mkulima anaweza kuhifadhi hadi Sh20,000 kila mwezi ama zaidi, ikitegemea kiwango cha sola anachoweza kunasa kila siku,” Muchai alisema.

Meneja wa kilimo kutoka Ujerumani Oliver Bowry kutoka shirika la OMYA, aliwafundisha wakulima jinsi ya kupunguza asidi nyingi mchangani, akiwashauri kutumia mbolea za kisasa zenye  kuongezea mchanga virutubishi muhimu.

Alilinganisha uzalishaji katika mataifa yaliyoendelea na Afrika akisema tofauti kubwa inatokana na utumiaji wa teknolojia ipasavyo.

“Teknolojia imeleta faida nyingi kuliko hasara.Mabadiliko ya hali ya anga,uchafuzi wa mazingira na ongezeko la idadi ya watu duniani ndiyo mambo yatakayowezesha bara la Afrika kushindana na ulaya,” Bowry alisema.

KARLO imekuwa ikiandaa makongamano kila mwaka ili kuwafikia wakulima wadogo mashinani wasiomudu gharama kubwa ya uzalishaji .

Kupitia mtandao wa kijamii pia wameweza kufanya kazi kwa ukaribu na mataifa ya kigeni kwa kupokezana mawazo.

You can share this post!

SAKATA YA HONGO BUNGENI: Wabunge 15 kuchunguzwa

Huenda rekodi ya Kipchoge isivunjwe hivi karibuni

adminleo