Habari Mseto

Kamati maalum ikague riba ya mikopo – Kuria

November 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na DAVID MWERE

MBUNGE wa Gatundu Kusini Moses Kuria amependekeza kubuniwa kwa kamati maalum ya bunge ya kukagua usimamizi wa uchumi nchini pamoja na viwango vya riba vinavyotozwa na benki na taasisi nyinginezo za kifedha kwa mikopo.

Mara litakapowasilishwa katika Bunge la Kitaifa, pendekezo hilo litasomwa ambapo Kamati ya Shughuli za Bunge (HBC) inayoongozwa na Spika Justin Muturi itatenga siku ya kutathmini mswada huo.

Kamati hiyo ya wanachama 15 itajumuisha Bw Moses Kuria (Mwenyekiti), David Mboni (Kitui Mashinani), Sam Atandi (Alego Usonga), John Sakwa Bunyasi (Nambale), Memusi Kanchori (Kajiado ya Kati), Buswamad Shariff Nassir (Mvita) na Kathuri Murungi (Imenti Kusini).

Wengine ni pamoja na Shakir Shabir (Kisumu Mashariki), Chris Wamalwa (Kiminini), Caleb Kositany (Sony), Purity Wangui Ngirichi (Kirinyaga), Beatrice Adagala (Vihiga), Rosa Buyu (Kisumu), Soipan Tuya (Narok) na Jessica Mbalu (Kibwezi Mashariki).

Hatua ya Bw Kuria hasa kuhusiana na viwango vya riba imejiri baada ya Bunge kukosa kufikisha idadi inayofaa ya kuzuia kubatilishwa kwa Kipengele 33B cha Sheria kuhusu Benki iliyowezesha kurejeshwa kwa riba.

Pendekezo la kubatilisha Sheria ya Benki lilijumuishwa katika Mswada wa Fedha, 2019, uliotiwa sahihi kama sheria mnamo Alhamisi na Rais Uhuru Kenyatta.

Sheria hiyo iliyobuniwa 2016 na Mbunge wa Kiambu Jude Njomo, ilidhamiriwa kuweka vidhibiti riba kwa viwango vya mikopo vya benki katika asilimia nne juu ya kiwango kinachotozwa na Benki Kuu (CBK) ili kuwalinda Wakenya dhidi ya mikopo yenye riba ghali na kunyanyaswa na benki.

Matokeo ya kubatilishwa kwa sheria hiyo yana athari kwa viwango vya riba na soko la fedha za mikopo, hali inayomaanisha kuwa benki zitafurahia uhuru wa kubadilisha masharti ya mikopo.

Notisi

Tayari baadhi za benki zimetoa notisi kwa waajiriwa wao kuhusu hatua inayolenga kubadilisha viwango vya riba.

“Kufuatia kutiwa sahihi kwa Mswada wa Fedha kuwa sheria na rais, benki imebadilisha viwango vya riba kwa bidhaa kadha kuambatana na viwango vya mikopo. Bei ya mikopo iliyopo itatangazwa hivi punde,” Mkurugenzi wa Benki ya Sidian, Chege Thumbi alisema katika notisi ya Novemba 8, 2019, iliyoelekezewa wafanyakazi wa Benki.

Kulingana na notisi ya Benki ya Sidian, mikopo kwa mashirika sasa itavutia riba ya kiwango cha asilimia 16, Biashara Ndogo ndogo na za Wastani (SMEs) asilimia 17, wateja, mikopo ya kiwango kidogo au isiyo na mdhamini, mikopo ya kawaida, pamoja na mikopo kupitia simu, asilimia 19 mtawalia.

Hata hivyo, Bw Kuria anasema ikiwa benki zitaendeleza unyanyasaji, atawasilisha tena udhibiti riba baada ya miezi sita kuambatana na kanuni ya Bunge inayosema kuwa urekebishaji wa sheria unaweza tu kuwasilishwa katika sheria mpya baada ya miezi sita.

“Ikiwa benki zitarejelea mikopo iliyopo kwa sasa, ikiwa zitakaidi na kupita asilimia 4 ya kiwango cha CBK, nitawasilisha marekebisho haya baada ya miezi sita,” akasema.