Kampuni ya Dawa Group yasaidia kaunti ya Kiambu kupambana na Covid-19
Na LAWRENCE ONGARO
KAMPUNI ya Dawa Group Limited ya Thika, imetoa dawa ya kunyunyuziwa ili kusaidia Kaunti ya Kiambu kukabiliana na janga la Covid-19.
Katika hafla fupi ya kukabidhi dawa hizo kwa kaunti ya Kiambu mwishoni mwa wiki jana, mkurugenzi wa kampuni hiyo Dkt Ajay Patel, alisema dawa hizo ni pamoja na sanitaiza.
“Sisi kama washikadau katika sekta ya afya tutazidi kushirikiana na kaunti ya Kiambu ili kuzidisha uhusiano mwema kwa maswala ya kiafya,” alisema Dkt Ajay.
Gavana wa Kaunti ya Kiambu Dkt James Nyoro alipongeza juhudi za shirika la Kenya Association of Manufacturers kwa juhudi za kusaidia kwa dhati hasa wakati huu mgumu wa janga la Covid-19.
“Tumepata misaada tofauti ya chakula kutoka kwa kampuni na mashirika na tunashukuru kwa hayo,” alisema Dkt Nyoro.
Alisema watafanya mazungumzo na benki tofauti ili kuzipa mikopo kampuni ambazo zimeathirika kibiashara.
Wakati huo pia kampuni ya Merek International, ilifanya juhudi ya kupuliza dawa ya kupunguza uwezekano wa maambukizi ya Covid-19 katika afisi za kaunti ndogo ya Thika.
Alisema hiyo ni njia mojawapo ya kukabiliana na Covid-19.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara mjini Thika Bw Alfred Wanyoike alipongeza wakazi wa Thika walio mstari wa mbele kwa kujitolea mhanga kusaidia waathiriwa kwa kuwapa chakula.
“Tutazidi kushirikiana na Kaunti ya Kiambu ili kudumisha ushirikiano mwema. Tayari usambazaji wa chakula mjini Thika umeendeshwa kwa uwazi na uwajibikaji chini ya uangalizi wa machifu na kamati ya Covid-19 Fund,” alisema Bw Wanyoike.