KANU yamtaka Ruto kuomba Moi radhi
Na ONYANGO K’ONYANGO
JUHUDI za wazee wa jamii ya Wakalenjin kuwapatanisha Naibu wa Rais William Ruto na Seneta wa Baringo Gideon Moi huenda zikagonga mwamba baada ya Katibu Mkuu wa Kanu, Nick Salat kumtaka Bw Ruto kwanza kumwomba msamaha Rais Mstaafu Mzee Daniel Moi.
Kwenye mahojiano na Taifa Leo Jumatano, Bw Salat alisema chama cha Kanu kiko tayari kupatana na Bw Ruto kuhakisha viongozi hao kutoka eneo la Bonde la Ufa wanaungana kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.
“Mwenyekiti wetu ambaye ni Seneta wa Baringo yuko tayari kufanya mazungumzo ya kupatanishwa na Bw Ruto. Lakini wazee ambao wamejitolea kuwapatanisha wanafaa kuelewa kiini cha mzozo baina ya wawili hao,” akasema Bw Salat.
“Kwanza kabisa, Bw Ruto anafaa kuomba msamaha Mzee Moi kwa sababu yeye ndiye amekuwa akitoa matamshi yasiyofaa dhidi ya familia ya Rais Mstaafu,” akaongezea.
Wazee wa jamii ya Wakalenjin hivi majuzi walionya kuwa huenda wakaambulia patupu katika kinyang’anyiro cha urais 2022 iwapo Bw Ruto na Bw Moi hawatazika tofauti zao na kuungana.
Kiongozi wa Baraza la Wazee la Myoot Meja (Mstaafu) John Seii alilalama kuwa juhudi zao za kuunganisha wanasiasa hao hazijazaa matunda kutokana na misimamo yao mikali.
Kulingana na Bw Seii, wazee hao hawajawahi kufanikiwa kukutana na viongozi hao wawili katika juhudi za kuwapatanisha. “Viongozi hao wawili wote ni watoto wetu. Tumejaribu kukutana nao kwa kuwatumia mialiko kupitia wasaidizi wao na hata kuwaeleza ana kwa ana katika mikutano ya umma, lakini wamekataa kutusikiza,” akasema Bw Seii.
Viongozi hao wamekuwa wakirushiana cheche za maneno katika siku za hivi karibuni hivyo kutatiza juhudi za kuwapatanisha. Bw Salati, hata hivyo, alisema Bw Moi hatashiriki mazungumzo iwapo lengo la wazee hao ni kumlazimisha kutupilia mbali azma yake kuwania urais 2022.