Karangi atolewa kijasho wanachama wa bodi ya NSSF kukwepa kikao na PIC bungeni
Na CHARLES WASONGA
MWENYEKITI wa Bodi ya wasimamizi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii na Mafao (NSSF) Julius Karangi alikabiliwa na wakati mgumu Jumanne kuelezea ni kwa nini wanachama wa bodi yake walikaidi mwaliko wa kufika mbele ya kamati ya bunge kuhusu uwekezaji (PIC).
Kutofika kwa wanachama wengine saba wa bodi hiyo kulisababisha wanachama wa PIC kuahirisha mkutano wao na Jenerali (Mstaafu) na wenzake na kuwaagiza warejee Jumatatu, Novemba 25, 2019.
Kati ya wanachama 10 wa bodi hiyo, ni wawili pekee, kando na mwenyekiti Jenerali (Mstaafu) Karangi, walioitikia mwaliko wa kufikia mbele ya kamati hiyo kujibu maswali kadhaa kuhusu masuala mbalimbali kuhusiana na usimamizi wa asasi hiyo. Vilevile, alikuwepo kaimu Afisa Mkuu Mtendaji Bw Anthony Omerikwa.
Wanachama wengine waliofika mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Sheriff Nassir ni aliyekuwa mbunge wa Laisamis John Lekuton na Profesa Dulacho Galgalo Barako.
Wale ambao hawakufika mbele ya kamati hiyo ya PIC ni pamoja na Katibu wa Wizara ya Leba Peter Tumm, Damaris Muhika, Marion Mutungi, Mark J. Obuya, Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini (Cotu-K) Francis Atwoli na Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirikisho la Waajiri Nchini (FKE).
“Kwa sababu ni wanachama watatu pekee waliofika, sheria haituruhusu kuendelea na kikao hiki. Kwa hivyo, Bw Mwenyekiti itabidi mrudi na muwashawishi wenzenu kuandamana nanyi Jumatatu, Novemba 25,” akasema Bw Nassir.
Naye mbunge wa Kiminini Chris Wamalwa alisema kutofika kwa wanachama hao wa bodi kunadhihirisha jinsi ambavyo hawachukulii kwa uzito wajibu wao katika NSSF.
Jeneralai Karangi aliwaambia wabunge hao kwamba ni wanachama wawili pekee wa bodi yake waliompigia simu wakiomba radhi kwamba hawangehudhuria.
“Na Katibu Mkuu Francis Atwoli amesafiri nje ya nchi katika ziara ya kikazi nchini Nigeria,” akasema Jenerali Karangi.
Thuluthi mbili
Kulingana na sheria ya NSSF, angalau thuluthi mbili ya wanachama wa bodi yake ya usimamizi ndiyo wanahitajika katika vikao vyake ili viwe halali. Kwa hivyo, wakati wa mkutano na kamati ya PIC katika majengo ya Bunge Jumanne bodi hiyo ilipasa kuwakilishwa na angalau wanachama saba.
Hii ndiyo sababu iliyofanya wabunge kudinda kuendelea na mkutano na kuwaamuru waondoke na warejee wakiwa idadi hitajika kwa mujibu wa sheria za hazina hiyo.
Hata hivyo, duru ziliambia Taifa Leo kwamba wanachama wa bodi hiyo walifeli kufika mbele ya wabunge “kimakusudi kwa sababu walijua suala la uteuzi wa Afisa Mkuu Mtendaji lingeibuliwa.”
“Mambo ni magumu katika NSSF kwa sababu wanachama wa bodi wako tu lakini wanakwepa kufika mbele ya kamati,” akasema meneja mmoja wa cheo cha juu ambaye aliomba tusichapishe jina lake.
“Hawatizami NSSF kama taasisi. Haja yao kuu ni kuhakikisha kuwa mtu wanayempendelea ndiye anashikilia wadhifa wa afisa mkuu mtendaji,” akasema.
Kumekuwa na mvutano mkubwa miongoni mwa wanachama wa bodi hiyo kwa muda wa zaidi ya miaka mitano hali iliyofanya kufeli kuteuliwa Afisa Mkuu Mtendaji wa kudumu.
Ni kutokana na mvutano ambapo Bw Omerikwa amekuwa akishikilia wadhifa huo kama kaimu kwa zaidi ya miaka mitano tangu mtangulizi wake Richard Langat afutwe kazi kwa tuhuma za ufisadi.
Isitoshe, wengi wa wasimamizi wengine wa hazina hiyo pia wanashikilia nyadhifa zao kama makaimu.
Mapema 2019 shughuli ya mahojiano ya kusaka atakayeshikilia wadhifa wa Afisa Mkuu Mtendaji ilifanyika katika hoteli ya Windsor Golf ambapo ilidaiwa kuwa Bw Omerikwa aliibuka bora.
Aghalabu nchini Kenya wengi wana mazoea ya kuita NSSF kuwa ni Hazina ya Kitaifa ya Malipo ya Uzeeni.