Karlo yazindua mbegu mpya ya mahindi
Na MWANGI MUIRURI
WAKULIMA wa mahindi hapa nchini watanufaika na aina mpya ya mbegu ambayo imezinduliwa kwa nia ya kuzidisha mazao katika maeneo baridi.
Mbegu hiyo ilizinduliwa Jumanne na idara ya utafiti wa kilimo cha mimea na uimarishaji mifugo (Karlo) tawi la Embu.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Dkt Stephen Njoka, mbegu hiyo kwa jina Embu Synthetic ni ya kipekee kwani mazao yake yanaweza yakapandwa tena kwa misimu mitano mtawalia kinyume na mbegu zingine ambazo hupoteza gredi ya mavuno iwapo utazipanda tena baada ya kuvuna.
“Kinyume na mbegu zinginezo za mahindi ambazo mazao yake huwezi ukayapanda tena kutoka gharani, hii unaweza hata kwa misimu 10 katika maeneoe ambayo huwa na misimu miiwli ya upanzi na mara tano kwa wakulima walio katika maeneo yaliyo na msimu mmoja wa upanzi kwa mwaka. Hivyo basi kuwapunguzia wakulima gharama ya ununuzi wa mbegu,” akasema Dkt Njoka.
Aidha, akaongeza, aina hiyo imethibitishwa kisayansi kuwa ekari moja inaweza kutoa magunia 35 ya mazao, kila gunia likiwa ni la kilo 90.
“Ukifanya hesabu ya mauzo, utapata kuwa kilo moja ya mbegu hii iko na gharama ya Sh145 na ndicho kiasi cha kupandwa kwa ekari moja. Magunia 35 utapata ni kilo 3, 150. Magunia 35 ukiyauza kwa bei ya Sh3,200 kwa kila moja utapata kuwa pato ni Sh112,000. Hayo ndiyo manufaa ya mbegu hii,” akasema.
Kupunguza hasara
Utafiti huu wa mbegu unaendeshwa kupitia vigezo vya hali ya hewa katika maeneo tofauti ili kuwawezesha wakulima kupunguza hasara ambayo huwakumba wanapopanda mbegu ambazo haziwezi kunawili katika maeneo mbalimbali.
“Tayari kilo 2,000 za aina hiyo ya mbegu zimesambazwa kwa wakulima wa hapa nchini,” Bw Njoka akasema.
Aidha, alisema aina hiyo ina uwezo wa kuhimili baridi na pia mvua ambayo mara kwa mara hukumba maeneo yenye kijibaridi.
Wakulima waliohudhuria hafla hiyo walielezewa kuwa aina hiyo ya mbegu huchukua miezi mitatu kukomaa na kuwa ina uwezo wa kustahimili magonjwa ambayo huandamana na hali ya kijibaridi.
“Juhudi hii ni ya kuimarisha uwezo wa wakulima wa hapa nchini kuafikia malengo yao ya ruwaza ya kiuchumi ya 2030 ambapo kila Mkenya anatarajiwa kuwa na mapato ya kadri,” akasema Bw Njoka.