• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
KASHFA YA NYS: Malumbano mahakamani

KASHFA YA NYS: Malumbano mahakamani

Na RICHARD MUNGUTI

KULIZUKA malumbano makali baina ya mawakili wanaowatetea washukiwa 37 katika kashfa ya Sh8bilioni ya shirika la huduma ya vijana kwa taifa (NYS) na viongozi wa mashtaka hata ikabidi hakimu aahirishe kesi kwa muda wa dakika 15.

Kizaazaa kilizuka pale wakili Assa Nyakundi alipomtaka kiongozi wa mashtaka Caroline Kimiri awache kuwasilisha tetezi mpya katika ombi la kupinga ushahidi mpya ukiwasilishwa katika kesi hiyo.

Mawakili kadhaa walimuunga mkono Bw Nyakundi wakisema ,” upande wa mashtaka wapasas kuzingatia tu sheria na wala sio kuwasilisha ushahidi mpya.”

Lakini Bi Kimiri alipandwa na mori na kumweleza hakimu mkuu Douglas Ogoti kuwa “mawakili hao wa kutetea washukiwa wako na njama ya kuhakikisha hakamilishi ushahidi wake.”

Hakimu alimtaka Bi Kimiri asisikize madai ya mawakili wa washukiwa kisha aendelee akamilishe ushahidi wake.

Shambulizi hilo dhidi ya Bi Kimiri liliingiliwa na viongozi wengine wa mashtaka Bi Evah Kanyuaira , Bi Hellen Mutellah, Bw Jalson Makori na Bw Joseph Gitonga Riungu.

“Lazima mawakili wa kutetea washtakiwa watupe muda wa kuwasilisha ushahidi wetu. Hatukuwavuruga walipokuwa wanatoa tetezi zao,” alisema Bw Makori.

Mkinzano ulitokotoka hata Bw Makori akaomba mahakama iamuru aliyekuwa katibu wa ugatuzi Bi Lillian Mbogo Omollo arudi kukaa kizimbani ahame viti vya mawakili wanaomwakilisha kwa vile ndiye anazua vurugu na kuwataka mawakili wapinge ushahidi wa Bi Kimiri.

Upande wa mashtaka uliomba mahakama ikubali ushahidi mpya ulioguduliwa na mkurugenzi wa kuchunguza jinai (DCI).

Lakini washtakiwa wanaomba mahakama ikatae kupokea ushahidi mpya unao onyesha jinsi mamilioni ya pesa yalivyolipwa  mmoja wa familia ya Ngirita kati ya 2008 na 2016.

Wakipinga kuwasilishwa kwa ushahidi huo, washukiwa hao walimweleza hakimu mkuu Bw Ogoti , kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) alikiuka kifungu nambari 50 cha katiba kinachomtaka afichue ushahidi wote kabla ya kesi kuanza kusikizwa.

“Ni jukumu la DPP kutimiza vipengee vyote vya Kifungu nambari 50 (2) (c) na (J) cha katiba kinachomtaka amkabidhi kila mshukiwa ushahidi kabla ya kuanza kusikizwa kwa kesi,” Bw Ogoti alifahamishwa.

Mawakili Assa Nyakundi, Migos Ogamba na  Stephen Ligunya walisema hatua ya DPP kuwasilisha ombi la kuwasilisha kwa ushahidi baada ya kesi kuanza kusikizwa ni ukandamizaji wa haki za washtakiwa.

Mawakili hao walisema ufichuzi wa DPP kwamba Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) hakuwa amepata nakala za malipo ya zaidi ya Sh50milioni kwa Bi Phyilis Njeri Ngirita washukiwa waliposhtakiwa sio sababu tosha ya kukubaliwa kwa ushahidi huo.

Bw Ligunya alisema inaeleweka kwa DCI kusema alisahau kuambatanisha ushahidi huo alipowashtakiwa washukiwa hao kutokana na wingi wa hati za ushahidi zilizopo.

Hata hivyo alisema, viongozi saba wa mashtaka wakiongozwa na Bw Riungu Gitonga, walikosea kutowaarifu washtakiwa kwamba kuna ushahidi uliokuwa umesahaulika na kwamba utawasilishwa.

“Shida kubwa ya DPP ni kunyamaza na kumbe kuna ushahidi muhimu uliokuwa umeachwa nje,” alisema Bw Ligunya.

Bw Ligunya anayemwakilisha aliyekuwa katibu mkuu Bi Lillian Mbogo Omollo anayeshtakiwa kwa kutumia mamlaka yake vibaya na kufanya njama za kuibia NYS zaidi ya Sh226milioni.

Mahakama ilifahamishwa kuwa Fomu nambari1340 na 1341 zilizoidhinishwa kumlipa Bi Lucy Njeri Ngirita hazikuwa katika seti ya nakala za mwanzo.

“Kutokabidhiwa nakala hizi kumetutatiza kuandaa utetezi wetu,” Bw Ligunya alisema.

Alipinga kuwasilishwa kwa ushahidi huo.

Bw Ogamba aliambia mahakama DPP alikuwa amekimya kama maji ndani ya mtungi kwamba ushahidi wote haukukabidhiwa washtakiwa.

“Kesi zinazowakabili washtakiwa hawa ni tatu na hati hizi za ushahidi  ni muhimu sana kwa washukiwa kuandaa ushahidi,” alisema Bw Ogamba.

Alisema Phyillis Njeri Ngirita ambaye ni mmiliki wa kampuni ijulikanayo kwa jina Njewanga Enterprises anakabiliwa na mashtaka ya kupokea mali ya umma na ulanguzi wa pesa.

Alisema mshtakiwa huyo pamoja na wenzake 36 wamekosewa na akaomba korti ikatalie mbali ushahidi huo akisema utaathiri pakubwa utetezi wao. Washtakiwa hao 37 wanakabiliwa na mashtaka 82.

Wamekanusha wakishirikiana na wengine ambao hawako mahakamani walifanya njama za kuilaghai Serikali zaidi ya Sh226milioni.

Bi Omollo amekana alimruhusu mfanya biashara Bi Anne Wambere Wanjiku Ngirita kupitia kwa kampuni yake Annwaw Investment Sh54,848,750.

Pia ameshtakiwa kwa kuruhusu dada wa Anne, Bi Lucy Wambui Sh 63,254,008 na Phyillis Njeri Sh50,970,500.

You can share this post!

Afueni kwa wanougua kansa

NASA ILIVYONASWA

adminleo