Habari Mseto

Katibu adai hongo ya Sh5 milioni katika zabuni ya maharagwe

April 19th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA amedai kwamba katibu mmoja mkuu amekuwa akidai hongo ya Sh5milioni ndipo amkubalie kuuzia Idara ya Kushughulikia Mikasa maharagwe ya misaada.

Bw Ibrahim Mohamoud amedai katibu  huyo ambaye hakumtaja kwa jina amekuwa akimzuia kupata zabuni.

Bw Mohammed amesema kwamba zabuni hiyo ilikuwa imetangazwa Januari 16 mwaka huu.

Katika kesi aliyowasilisha mahakama kuu , mfanyabiashara huyo anaomba mahakama izime ununuzi huo wa maharagwe hayo ya kutoa msaada hadi kesi aliyoshtaki isikizwe na kuamuliwa.

Bw Mohammed amedai hongo hiyo inaitishwa na Bw Joseph Mukombe Ndolo kwa niaba ya katibu huyo ambaye ni ndugu yake.

Mlalamishi aliwasilisha kesi hiyo kupitia kwa kampuni yake kwa jina Indigo Capital Services.

Amesema kampuni hiyo imetishwa kuzuiliwa kushiriki katika zabuni hiyo endapo hatatoa kiinua mgongo hicho.

Lakini katibu huyo na mwanasheria mkuu wamepinga kesi hiyo ikisikizwa na kitengo cha kuamua kesi za masuala ya ukiukaji wa haki.

Wakili wa Serikali Lumiti Chilaka amesema suala la madai ya hongo yanapasa kushughulikiwa na polisi na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP).