Kaunti 36 hatarini kutafunwa na makali ya njaa
Na CAROLYNE AGOSA
SERIKALI Jumatano ilitoa tahadhari ya kuzuka kwa baa la njaa katika kaunti 36 nchini zinazokabiliwa na hali ngumu ya ukame.
Tahadhari hiyo iliyotumwa kwa vyombo vya habari ilisema kuwa kaunti tisa ziko katika hali mbaya huku zingine 13 zikionyesha dalili ya kuelekea pabaya.
Taarifa hiyo ilitokana na ripoti ya Mamlaka ya Kitaifa ya Kukabiliana na Baa la Njaa (NDMA) inaonyesha kuwa kaunti zingine 14 pia zinakumbana na ukame, ingawa hali ya ukame haijafikia viwango vilivyoshuhudiwa mwaka jana.
“Ripoti ilionyesha kuwa kaunti 14 zinashuhudia hali ya kawaida ya ukame huku tisa zingine zikiwa katika hali mbaya. Aidha, hali inaelekea kuwa mbaya katika kaunti 13 ambazo ni pamoja na Garissa, Isiolo, Kitui, Marsabit, Samburu, Tana River, Turkana, Wajir, Kilifi, Laikipia, Mandera, Nyeri (eneo la Kieni) na Pokot Magharibi,” ilisema tahadhari hiyo.
Iliongeza: “Serikali imeweka mikakati ya kukabiliana na ukame ili kuzuia madhara yake kwa masomo na hali ya maisha nchini.”
Tahadhari hiyo ilitolewa baada ya kikao cha kamati ya pamoja ya wizara saba husika, kilichofanyika katika jumba la Harambee mjini Nairobi.
Kamati hiyo iliongozwa na Waziri wa Usalama na Uratibu wa Serikali ya Kitaifa Dkt Fred Matiang’i. Mawaziri wengine waliohudhuria ni Sicily Kariuki (Afya), Najib Balala (Utalii), Balozi Amina Mohamed (Elimu), Mwangi Kiunjuri (Kilimo), Simon Chelugui (Maji) na Eugene Wamalwa (Ugatuzi).
Miongoni mwa hatua zilizoafikiwa kwenye mkutano huo wa mawaziri ni ukusanyaji wa fedha za kutoa chakula cha msaada kwa waathiriwa na vile vile dawa zaidi za matibabu kutumwa katika maeneo husika.
“Chakula cha dharura, maji na bidhaa zingine muhimu zitatolewa kwa nyumba, jamii na taasisi mbalimbali zilizoathirika, ikiwemo shule,” ilieleza taarifa.
Serikali pia itashirikiana na wadau kuimarisha usalama, kudumisha amani na pia mikataba ya maelewano kuhusu ugavi wa rasilimali katika maeneo yenye kuzuka vita ili kuzuia mizozo na mashambulizi yanayotokana na ukosefu wa chakula.
“Mikakati hii inajumuisha uimarishaji wa huduma za afya za mifugo ili kuwakinga wafugaji na hasara ya kupoteza wanyama wao; ujenzi wa visima vya maji mbugani kuzuia mizozo ya wanyamapori na binadamu; kutoa ruzuku ya mafuta kwa visima vinavyotumia pampu kusambaza maji; na kusambaza chakula cha ziada cha mifugo,” ilisema kamati.