Kaunti saba kunyimwa Sh2.2 bilioni kutoka Denmark
Na ANGELA OKETCH
KAUNTI saba ziko katika hatari ya kuondolewa katika orodha ya kaunti ambazo zitafaidika kwa msaada wa Sh2.2 bilioni kutoka kwa serikali ya Denmark, kwa kukosa kutumia kikamilifu fedha zilizopewa awali. Kaunti hizi zinalaumiwa kwa kukosa kutoa ripoti za uhasibu kuonyesha zilivyotumia fedha hizo.
Kwenye barua kwa Baraza la Magavana (CoG) mnamo Jumanne, Shirika la Kitaifa la Maendeleo la Denmark (Danida) lilisema kuwa ukaguzi wake umebaini kwamba kaunti saba hazijatumia fedha zilizotengewa wala hazijazisambaza kwa hospitali za kiwango cha Level 3 na 4.Barua hiyo iliangazia Mpango wa Afya kwa Wote (UHC).
Shirika hilo pia lilieleza kuwa baadhi ya kaunti hazijatoa ripoti yoyote kuhusu zilivyotumia fedha hizo.Kenya ilipokea msaada wa Sh2.2 bilioni kutoka kwa shirika hilo kufadhili huduma za afya katika kaunti mbalimbali nchini.
Kaunti ya Trans Nzoia haijatumia Sh486,000, hicho kikiwa kiwango kikubwa zaidi cha fedha ambazo hazijatumiwa miongoni mwa kaunti zinazokabiliwa na tatizo hilo. Kaunti nyingine ni Homa Bay, Sh115,000 huku Kwale ikiwa haijatumia Sh14,000.
Kaunti za Kilifi, Meru na Nairobi hazijawasilisha ripoti kuhusu jinsi fedha hizo zilivyotumiwa. Kaunti ya Kiambu pia ilikuwa na tatizo la fedha zilizobaki, hivyo huenda ikakosa kufaidika kwa ufadhili huo.Baadhi ya kaunti ambazo zinatarajiwa kupokea fedha hizo ni Garissa, Taita Taveta, Tana River, Mandera, Lamu na Mombasa.
Kaunti ya Mombasa, hata hivyo, inaendelea kufanyiwa utathmini.Kwa mujibu wa shirika la uhasibu la Ernest & Young, ambalo linafanya ukaguzi kuhusu matumizi ya fedha hizo kwa niaba ya Danida, shughuli hiyo haikuweza kukamilika kwani baadhi ya kaunti hazikutoa maelezo ya kutosha.
Kaunti nyingine hazikuwasilisha ripoti zozote za uhasibu.Ripoti hiyo ilionyesha kuwa kaunti 40 zilitimiza viwango vyote vya uhasibu vinavyohitajika, hivyo zitapokea fedha hizo kati ya Julai na Desemba mwaka huu.
“Hata hivyo, wahasibu walibaini kwamba kaunti saba, ikiwemo Isiolo hazijatimiza masharti yafaayo kupokea ufadhili huo. Isiolo ilijumuishwa kwenye orodha hiyo kwa kutoitengea idara ya afya fedha za kutosha kwenye bajeti yake,” ikaeleza ripoti