Kaunti ya Garissa matatani kwa kutolipa wakandarasi pesa zao kwa miaka saba
Na FARHIYA HUSSEIN
SERIKALI ya Kaunti ya Garissa imejipata matatani kwa kutolipa wakandarasi pesa zao kwa miaka saba ambazo ni malimbikizo ya Sh2.3 bilioni.
Katika barua iliyoelekezwa kwa Wizara ya Fedha, wakandarasi wanasema walifanya miradi kadhaa kwa serikali ya kwanza na hakuna malipo ambayo wamepokea.
“Tulitarajia serikali ya pili ingesimamia mali na madeni yote ya serikali iliyopita. Lakini tumechukuliwa kama hatuna maana na hatujapokea pesa zetu,” ilisoma ripoti ambayo Taifa Leo imeona.
Akithibitisha suala hilo, mwenyekiti wa wakandarasi kaunti hiyo, Bw Azzid Yusuf alisema waliandika barua kadhaa kwa serikali ya kaunti na hakuna majibu waliyopata na ndiyo sababu kuu ya wao kuandikia Wizara ya Fedha.
“Hatujapata hela zozote kutoka mwaka 2013 hadi sasa. Kulikuwa na ripoti iliyofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali mnamo Juni 2018 ikisema kwamba wakandarasi wa Kaunti ya Garissa wanasubiri pesa zao Sh2.3 bilioni,” akasema Bw Yusuf.
Anaongeza kuwa kila mara gavana wa kaunti hiyo akiitishwa malipo anasema “hii ni serikali mpya na tunataka kushughulikia miradi mipya.”
“Hakuna miradi yoyote mipya inayoendelea hapa katika Kaunti ya Garissa. Hii ni katika kujaribu kukwepa kulipa madeni. Gavana alifanya bajeti mwaka huu na kuamuru kikao cha bunge kiandaliwe ili kipitishe. Lakini bado hatujapata malipo yoyote,” anasema Bw Yusuf.
Barua hiyo iliyoandaliwa na wakandarasi ilitumwa Ijumaa wiki jana huku Gavana wa Garissa, Katibu wa Kaunti, Mdhibiti wa Bajeti, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Idara na Idara zingine zinazohusiana, walitumiwa nakala.
Akizungumza na Taifa Leo kwa njia ya simu, Katibu wa Kaunti ya Garissa Abdi Ali alithibitisha kuwa walipokea barua hiyo siku ya Ijumaa.