Habari Mseto

Kaunti ya Nairobi kutumia Sh100 milioni kuangamiza mbwa koko jijini

May 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA DANIEL OGETTA

KAUNTI ya Nairobi imeshtua Wakenya kutangaza kuwa itatumia Sh100 milioni kuwaua mbwa koko katika kipindi cha mwaka mmoja.

Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Bw Muriithi Muhari alisema kwamba jiji la Nairobi lina zaidi ya mbwa koko 50,000.

“Mbwa hawa huwasumbua wakazi wa Nairobi hasa wanaofanya biashara jijini, huwauma wanafunzi wanapoenda shuleni na wakati mwingine, husababisha ajali za barabarani,” alisema.

Aliongeza kuwa jiji linakumbwa na idadi kubwa ya mbwa koko huku wadi 70 za kaunti hiyo zikiathirika zaidi.

Bw Muriithi alisema kwamba watakuwa na ‘utu’ hata wakati wa kuwaangamiza mbwa hao kwani watatumia bunduki zinazotumika kuwaua ng’ombe vichinjioni.

“Kuwaua mbwa hawa kwa kuwapiga risasi hata limekubalika na shirika la afya duniani,” alisema Muriithi.

Alisema Sh100 milioni zitatumika kununua bunduki hizi za kuwaua mbwa koko na kuupanua nyanja za kuwazika mbwa hawa.

Bw Muriithi ambaye alikuwa akizungumza katika kongamano la World Animal Protection (WAP) katika hoteli moja jijini Nairobi alieleza kwamba zaidi ya kesi 6,000 za kuumwa na mbwa na hata majeraha kutokana mbwa koko hawa zimeripotiwa.

“Kati ya 2018 na 2019, tumezipokea ripoti za vifo vya watoto watano kutokana na kichaa cha mbwa koko hawa.”

Bw Muriithi alisema kwamba watashirikiana na WAP kufanya kampeni za kuhamasisha umma kuhusu utunzaji wa mbwa.

“Kuna sheria za kuwaruhusu wakazi kuwafuga mbwa mradi uwe katika mazingira yafaayo na afya na maslahi yao kutunzwa vyema,” alisema.

Kulingana na Bi Emily Mudoga wa shirika la utunzaji wa wanyama, wakazi wa Nairobi wamekuwa wakikiuka sheria za kuwalea mbwa hivyo basi kuwaacha kutapakaa jijini.

Bi Mudoga alisema kwamba ripoti zinonyesha kwamba asilimia 50 ya wakazi wa mitaa ya Karen, Kibera na Kawangware huwaacha huru mbwa wao usiku.

“Tunahitaji kushirikiana na kujadiliana pamoja kupata njia mwafaka ya kusuluhisha janga hili hususan hapa Nairobi,” alisema.