Kaunti yadaiwa kumwaga Sh600m kwa miradi hewa
Na COLLINS OMULO
SERIKALI ya Kaunti ya Nairobi inayosimamiwa na Gavana Mike Sonko, inashukiwa ilitumia zaidi ya Sh600 milioni kwa miradi hewa.
Imebainika utumizi huo huenda ulifanywa kwa miezi sita ya kwanza ya mwaka wa fedha uliokamilika Juni.Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya Msimamizi wa Bajeti ya Taifa kuhusu utekelezaji wa bajeti za kaunti.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kaunti ilishindwa kutoa orodha ya miradi ambayo ilidai kutekeleza kwa kipindi hicho licha ya kuwa Sh632.1 milioni zilitumiwa.
‘Kiasi hicho cha fedha ni asilimia 5.6 ya bajeti ya maendeleo ya mwaka ambayo ilikuwa Sh11.27 bilioni,’ ikasema ripoti hiyo.
Kinachoshangaza ni kuwa, wakati huo, kiwango cha fedha ambacho kaunti ilitumia kwa safari za humu nchini kiliongezeka mara mbili ikilinganishwa na ilivyokuwa katika kipindi cha fedha cha mwaka uliotangulia.
Ripoti hiyo ilionyesha kuwa, Sh337.9 milioni zilitumiwa kwa safari, ilhali mwaka uliotangulia Sh157.35 milioni ndizo zilikuwa zimetumiwa.
Afisi ya Gavana Sonko ilitumia Sh232.39 milioni kutoka kwa kiwango hicho, huku bunge la kaunti likitumia Sh105.5 milioni.