Kaunti za Pwani zaanza kukabiliana na baa la njaa
Na SAMUEL BAYA
BAADHI ya kaunti za Pwani sasa zimeanza kujiandaa vilivyo kukabiliana na baa la njaa na kiangazi.
Tayari serikali ya kaunti ya Kilifi jana ilisema kuwa imeomba Sh50 milioni zaidi ili kuiwezesha kununua chakula cha kutosha kusambazia wenye njaa.
Akiongea na Taifa Leo kwa njia ya simu, afisa wa kukabiliana na mikasa ya dharura Bw Adan Mohamed alisema kuwa wameomba bunge la kaunti hiyo kuhidinisha fedha hizo ili kuokoa maisha ya wakazi.
“Tumekuwa na shughuli za kugawa chakula cha zaidi ya Sh30 milioni katika maeneo mbalimbali ya kaunti ambayo yamekumbwa na kiangazi,” akasema Bw Mohamed.
Aidha afisa huyo alisema kuwa mbali na kuwapatia waathiriwa chakula, vilevile wamekuwa wakiendeleza mpango wa kuwalipa wazee na watoto wasiojweiza katika jamii Sh2,000 kila mwezi.
“Lengo letu hasa ni watu Sh50 kufaidika kila wadi katika awamu yetu ya kwanza. Kufikia sasa tumesaidia wakazi Sh1,300 huku lengo letu ikiwa ni kuwahudumia jumla ya wakazi 1,750,” akasema afisa huyo.
Naibu kiongozi wa walio wengi katika bunge la kaunti hiyo Bw Sammy Ndago, alithitisha kuwa bajeti hiyo ya ziada ilikuwa imefikishwa katika bunge la hilo. Alisema kuwa huenda ikaanza kujadiliwa kwa haraka wiki ijayo.
“Tunajua kwamba bajeti ya ziada kukabiliana na baa la njaa ililetwa na kwa sababu kuna uharaka ndani yake, tunatarajia kwamba itaanza kujadiliwa wiki ijayo,” akasema Bw Ndago.
Mbunge wa Ganze Bw Teddy Mwambire alisema kuwa hali imeanza kuwa mbaya katika maeneo ya Bamba, Ganze, Jaribuni na Vitengeni.
“Ninaamini kwamba huduma za dharura zinahitaji lakini pia, lazima tuangalie njia za muda mrefu za kumaliza tatizo hili,” akasema Bw Mwambire.
Waziri wa Kilimo katika kaunti ya Kwale Bi Joan Nyamasio alisema kuwa taarifa za awali zinaonyesha kwamba kaunti hiyo haiko katika hatari ya baa la njaa.
“Tulifanya utafiti wetu na kugundua kwamba kwa sasa hatuko vibaya sana. Lakini hata hivyo hatujatulia ila tunaangalia kwa makini matukio yanavyoendelea,” akasema Bi Nyamasio.
Naye Kamishna wa kaunti ya Kilifi Bw Magu Mutindika alisema kuwa ripoti zote za utafiti kuhusu ukame na baa la njaa zimetumwa kwa afisi ya mshrikishi mkuu wa Pwani Bw John Elungata ili zishughulikiwe kuanzia huko.
“Sisi tulitayarisha ripoti zetu na kwa sasa ziko kwa afisi ya mshirikishi wetu Bw Elungata.
Yeye ndiye ambaye atakuwa katika wakati mzuri kutoa tathmini ya hali ilivyo kwa sasa,” akasema Bw Mutindika.
Alipohojiwa kwa njia ya simu na Taifa Leo, Bw Elungata alisema kuwa bado wanaendelea kuangalia ripoti hiyo na kwamba waandishi watajulishwa wakati mwafaka ikitolewa.
“Ripoti bado hajakamilika. Bado tunaishughulikia kwa hivyo wakati wowote ikiwa tayari, basi tutawajulisha,” akasema Bw Elungata.