Kaunti za Pwani zatahadharisha wakazi kuhusu mafuriko yajayo
Na WACHIRA MWANGI
WAKAZI wa pwani ambao wanaishi maeneo yanayokumbwa na mafuriko, wametahadharishwa wahamie maeneo ya miinuko huku magavana wa kaunti za eneo hilo wakianzisha mipango ya kutafuta suluhu ya mafuriko, kabla ya msimu wa mvua ya masika kuanza.
Maafisa wa serikali za kaunti wamesema kuwa hawatasaidia yeyote ambaye atakosa kutii tahadhari na kuhamia maeneo ya juu.
“Afisi ya gavana tayari imetahadharisha wakazi wanaoishi maeneo ya chini kabla ya mvua. Hatutafidia mkazi yeyote ambaye ataendelea kukaa huko. Watu wengi wanaishi kando ya mito na hivyo wako kwenye hatari endapo itavunja kingo,” alisema mkurugenzi wa mawasiliano Kaunti ya Tana River, Steve Juma.
Baadhi ya maeneo yameanza kushuhudia mvua ilivyotabiriwa na idara ya utabiri wa hewa, mvua ambayo inatarajiwa kuendelea hadi Juni.
Katika Kaunti ya Mombasa, serikali ya kaunti inatengeneza mitaro ya kusafirisha maji na kukarabati iliyopo sasa, ikijiandaa kwa mvua inayotarajiwa mwezi huu.
Gavana Hassan Joho amesema kuwa serikali ya kaunti inataka mvua zikianza kuwe na miundomsingi bora ili wakazi wasitatizike.
Gavana Salim Mvurya wa Kwale naye amethibitisha kuwa kaunti yake iko tayari kwa msimu wa mvua, akisema maafisa wake wako tayari kukabili hali katika maeneo ya Msambweni, Ramisi, Lunga lunga na Vanga ambayo huathirika na mafuriko sana.
“Aidha, tumejiandaa na mbinu za kukabili magonjwa yanayosababishwa na maji ili kuhakikisha kuwa wakazi hawateseki msimu huo,” Gavana Mvurya alisema.